Tone

Tone
Home » » MUUMINI AOMBA MWONGOZO HOFU YA EBOLA

MUUMINI AOMBA MWONGOZO HOFU YA EBOLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

LICHA ya Serikali kusisitiza ugonjwa wa ebola haujaingia nchini, hofu juu ya ugonjwa huo imeendelea kutanda, kiasi cha waumini wa Kanisa Katoliki, Kigango cha Nundu katika Parokia ya Nyakato jijini Mwanza kulazimika kuomba mwongozo wa Kanisa juu ya namna ya kuepuka kugusana wakiwa kanisani.
Hali hiyo ilijitokeza jana katika kanisa hilo, baada ya Paroko wake, Padri Daniel Nana kuwaeleza waumini juu ya ujumbe alioupata kutoka kwa mmoja wa waumini juu ya tishio la ebola.
Akiwa amesimama mbele ya waumini wakati wa ibada mwishoni mwa wiki, alisema alipokea ujumbe kutoka kwa muumini ambaye hakujitambulisha jina akitaka mwongozo wa kanisa juu ya utaratibu wa waumini kutakiana amani kwa kupeana mikono wakiwa kanisani.
“Nimepokea ujumbe wa mmoja wa waumini akiniuliza Padri, sasa tutafanyaje wakati wa kutakiana amani kanisani kwani tunaambiwa kupeana mikono kunaambukiza ebola kwa kasi kubwa,” alisema Padri Nana akikariri ujumbe mfupi wa simu alioandikiwa na muumini wake.
Taarifa juu ya ujumbe huo wa simu ilipokelewa kwa vicheko na miguno kutoka kwa baadhi ya waamini ingawa baadhi yao walionesha kumuunga mkono mwenzao kwa kutikisa vichwa.
Ishara ya kutakiana amani kwa kupeana mikono imedumu ndani ya Kanisa Katoliki kwa miaka mingi ikiwa ishara ya kusambaza ujumbe wa amani na upendo ikiaminika ni maagizo ya Yesu Kristo wakati akizungumza na wafuasi wake kwa mujibu wa maandiko.
Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya kwanza kanisani hapo jana, Padri Nana alisema utamaduni wa kupeana amani kwa kushikana mikono haukuwa na mbadala na akaongeza waumini wenye wasiwasi wa ebola wanaweza kukumbatiana na ama kubusiana wakitaka.
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana kuwasisitizia waumini umuhimu wa kuyaishi maagizo ya Yesu juu ya upendo na amani, aliwaelekeza waumini hao kuchagua kati ya njia hizo tatu kwa watakaopenda yaani kupeana mikono, kubusiana ama kukumbatiana wakiwa kanisani.
Kwa muda sasa hali imekuwa tete mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kufuatia uvumi ulioenezwa juu ya uwezekano wa kuwako mlipuko wa ebola kwenye baadhi ya maeneo ya mikoa hiyo.
Hata hivyo, uvumi uliodai Salome Richard (17) wa Sengerema alifariki dunia kwa ugonjwa wa ebola umekanushwa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo aliyekuwa amefuatana na wataalamu wa afya mkoani Mwanza katika mkutano wake na waandishi wa habari, mkutano uliolenga kuwatoa hofu wananchi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, Salome alifariki kwa ugonjwa wa malaria ingawa vipimo vingine kikiwemo cha ebola majibu yake hayajatoka rasmi.
“Ushahidi wa mazingira unaonesha marehemu alikufa kwa tatizo tofauti na ebola vinginevyo hali ingekuwa mbaya sana sasa hivi kuanzia huko nyumbani kwao, daladala aliyopanda na wote waliomsaidia mpaka hospitali,” alisema Ndikilo.
Alisema taarifa zilizopo zinaonesha wote waliomgusa Salome wakati wakimbeba kutoka eneo moja hadi jingine bado wako salama ingawa wataalamu wa afya wamechukua vipimo na kuzingira baadhi ya maeneo ili kujiridhisha zaidi.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza (RMO), Dk Valentino Bangi alisisitiza wakati akizungumza na gazeti hili jana kuwa, mkoa uko salama na tishio la maambukizi ya ugonjwa hatari wa ebola na magonjwa mengine ya hatari na kuwataka wananchi watulie na kusubiri maelekezo ya kitaalamu juu ya magonjwa hayo.
Pamoja na juhudi za watendaji hao mkoani Mwanza za kuwaelimisha wananchi, Serikali nayo imekuwa ikisisitiza kutokuwepo kwa ugonjwa huo nchini, huku ikichukua tahadhari za kila aina katika kukabiliana na ugonjwa huo endapo utatokea.
Mbali ya kusambaza vifaa vya kisasa vya kutambua ugonjwa huo katika mipaka yote nchini, viwanja vya ndege, katika bandari na maeneo mengine yenye mikusanyiko, serikali imetawanya pia wataalamu zaidi ya 13,000 kote nchini, achilia mbali kutenga hospitali maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa ebola wilayani Temeke endapo watatokea.
Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa