Home » » KAMATI YA SIASA SENGEREMA YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO

KAMATI YA SIASA SENGEREMA YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO



Na: Richard Bagolele - Sengerema

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilayani Sengerema imeridhishwa na ubora wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ambapo wamewataka wataalamu wanaosimamia miradi hiyo kuongeza umakini katika usimamizi ili miradi hiyo iwe na tija kwa jamii.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo wajumbe hao wamewataka wataalamu katika kila sekta kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa yenye ubora na thamani ya fedha iliyotumika iweze kuonekana.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Mark Agustine Makoye amesema katika miradi yote iliyotembelewa na kamati hiyo kwa kiasi kikubwa wameridhishwa na ubora wa mradi hiyo, hivyo amewataka watalaamu kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa wilayani Sengerema inasimamiwa vyema    na thamani ya fedha iweze kuonekana.

"Tumekagua na kufanya tathimini katika miradi yote tuliyotembelea, zaidi ya asilimia sabini ya miradi inaenda vizuri" amesema Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema.

Wakikagua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Nyamazugo wajumbe hao wamepongeza ubora wa mradi huo na wameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha mradi huo unafanyiwa marekebisho ya mapungufu yote yaliyojitokeza ili thamani ya fedha katika mradi huo iweze kuonekana.

Wajumbe hao pia wameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanakamilisha mapungufu yote yaliyopo katika hospitali ya Wilaya ya Sengerema iliyopo Mwabaluhi  ikiwemo matengenezo ya  barabara inayoelekea hospitalini hapo, njia za watembea kwa miguu katika hospitali hiyo pamoja na vifaa tiba ili hospitali hiyo ianze kutoa huduma kwa mapema iwezekanavyo.

Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu ameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha mazingira ya hospitali hiyo yanakuwa safi muda wote pamoja na uwepo wa njia za watembea kwa miguu na zenye kurahisisha uhamishwaji wa wagonjwa ndani ya hospitali hiyo.

Miradi mingine iliyotembelewa na kamati hiyo ni pamoja na Matengenezo ya Barabara ya Tabaruka-Buyagu, ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa sekondari ya Buyagu, ujenzi wa nyumba ya watumishi Zahanati ya Bitoto, ujenzi wa matundu 26 ya vyoo shule ya msingi Mweli na mradi wa maji Sima.


0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa