Home » » SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WANAOKIUKA SERA YA CHAKULA SHULENI

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WANAOKIUKA SERA YA CHAKULA SHULENI

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amewataka Wakuu wa Shule, Maafisa Elimu Kata na Viongozi wote wanaratibu na kusimamia sera ya chakula shuleni kuhakikisha wanaiendeleza sera ya kutoa chakula kwa wanafunzi pindi wawapo shuleni na wale ambao wanakiuka kampeni hiyo basi taarifa zitolewe ili waweze kuchukuliwa hatua.

Balandya ametoa tamko hilo julai 30, 2024 alipokuwa akiongoza kikao cha kamati ya lishe ngazi ya Mkoa kilicholenga kuboresha afya kwa watumishi na wananchi, Ambapo amewataka Viongozi hao wa afya ngazi ya Mkoa kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na serikali ikiwemo kuisimamia kwa ufasaha sera ya chakula shuleni.

Aidha, Katibu Tawala huyo amewataka watumishi wa Afya ngazi ya Mkoa kuhakikisha wanasimami sekta ya mazoezi pia kwa kuwa ndio msingi wa afya imara na katika kusisitiza hilo ametaka kuwepo na vipindi maalumu vya mazoezi kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

"Mnaweza mkatenga hata siku tatu kwa wiki, kila siku mtakayoichagua jioni mara baada ya muda wa kazi mkawa na kipindi cha mazoezi kwa watumishi wa hapa ofisi ya Mkuu wa Mkoa". Amesema Balandya wakati akisisitiza kuhusu kufanya mazoezi.

Kadhalika Bw. Balandya ametumia kikao hicho pia kuwataka Viongozi hao wa Afya ngazi ya Mkoa kuhakikisha wanatoa elimu ya matumizi sahihi ya chupa za maji za plastiki ambapo kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mtindo wa kutumika tena huku zikiwa tayari zimeshatumika na kwa namna zilivyotengenezwa hazikupaswa kutumiwa tena na hivyo zinaweza kuleta madhara kwa afya.

"Niwatake pia mkatoe elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya chupa ambazo zimekwishakutumika ni hatari kwa afya, hivyo mkawaambie wananchi huko anaweza akaitoboa chupa hiyo mara baada ya kuitumia ili kuifanya chupa hiyo isitumike tena". Amesema Balandya.

 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa