Home » » WAZIRI NDUMBARO AWEKA JIWE LA MSINGI UWANJA WA MICHEZO SENGEREMA

WAZIRI NDUMBARO AWEKA JIWE LA MSINGI UWANJA WA MICHEZO SENGEREMA


•⁠  ⁠Uwanja sasa kuitwa TABASAMU

•⁠  ⁠Sengerema Sekondari Kunufaika Miundombinu ya Michezo
*
Na: Richard Bagolele - Sengerema

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Julai 3, 2024 ameweka jiwe la Msingi wa ujenzi wa Uwanja wa Mnadani uliopo mjini Sengerema ambapo kupitia hotuba yake ameupa jina  Uwanja huo na kuwa uwanja wa Tabasamu kutokana na mchango mkubwa wa kufanikisha ujenzi huo uliotolewa na Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu kupitia fedha za mfuko wa Jimbo.

Akiongea katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi iliyofanyika uwanjani hapo Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema kupitia juhudi za Mbunge, Halmashauri na wadau wengine ni vyema uwanja huo ukapewa jina la Tabasamu kwani amekuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa uwanja huo na ametumia fedha za mfuko wa jimbo pamoja na mchango wake binafsi kufanikisha ujenzi wa uwanja huo ambapo pia amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji kuandaa andiko la maombi ya fedha litakalowasilishwa Wizarani ili kuweza kusaidia kukamilisha ujenzi wa uwanja huo.

"Na mimi leo naubadilisha jina huu uwanja huu wa Mnadani na kuitwa uwanja wa Tabasamu, Mhe. Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri na ninyi wananchi mmefanya jitihada kubwa kufanikisha ujenzi wa uwanja huu" amesema Dkt. Ndumbaro.

Awali Waziri Dkt. Ndumbaro alitembelea Sekondari ya Sengerema ambapo Serikali imepanga kujenga miundombinu mbalimbali ya michezo ikiwa ni miongoni mwa shule 56 za michezo zitakazojengwa nchini.

Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu amesema ujenzi wa uwanja huo kwa awamu ya kwanza ulianza tarehe 1 Aprili, 2024 na unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 360 ambapo ujenzi umefikia asilimia 75.

Amesema awamu ya pili ya ujenzi uwanja huo itakuwa ni ujenzi wa eneo la kuchezea na pamoja na uwekaji wa majukwaa ya watazamaji pamoja na taa za uwanjani kwa awamu ya tatu hivyo amemshukuru mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na amemwomba Waziri Dkt. Ndumbaro kupitia Wizara ya Michezo kusaidia ukamilishaji wa uwanja huo ambao unazo sifa zote za kuwa uwanja wa kisasa na ambao unaweza kutumika katika michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Mark Agustine Makoye amesema ujenzi wa uwanja wa michezo katika mji wa Sengerema ni hitaji la muda mrefu kwa wananchi hivyo amewaomba wananchi wa Sengerema kuwa tayari kuutumia uwanja huo ambapo vipaji  vingi vya wanamichezo vitaibuliwa.

 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa