Home » » WATAALAM WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUFANIKISHA AJENDA YA LISHE MASHULENI

WATAALAM WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUFANIKISHA AJENDA YA LISHE MASHULENI


Wataalam wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha ajenda ya lishe inatekelezeka na kufanikiwa katika shule zote za manispaa hiyo.

Rai hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela Dkt.Maria Kapinga wakati akizungumza na watendaji wa kata,mitaa na maafisa elimu kata katika ukumbi wa jengo jipya la utawala ambapo amefafanua kuwa ili suala la lishe mashuleni liweze kufanikiwa ni lazima wataalam hao waunganishe nguvu kwa pamoja kwa kuishirikisha jamii .

‘.. Ajenda ya lishe ni ajenda ya Mheshimiwa Rais, kwa hiyo sisi sote tuna jukumu la kuhakikisha ajenda hii inafanikiwa na watoto wanakuwa na afya bora, kuanzia wale wachanga mpaka wanafunzi wale wa mashuleni, mtoto hawezi kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri kama afya yake ni dhaifu ..’ Alisema

Aidha Dkt.Kapinga amewahakikishia ushirkiano wataalam wote wa sekta nyingine kwa muda wote wataohitaji kufanya hivyo ili kuhakikisha zoezi la lishe mashuleni linafanikiwa .

Mwl.Marco Busungu ni Afisa elimu msingi Manispaa ya Ilemela yeye amewataka wataalam hao kujituma na kutanguliza uzalendo katika kutekeleza majukumu yao kuhakikisha masuala ya lishe  yanafanikiwa na kwamba kwa mwaka huu wa fedha zipo jitihada ambazo serikali imezichukua katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya uratibu wa shughuli za lishe kwa watendaji wa mitaa na kata .

Nae Mratibu wa lishe Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khasimu amesema kuwa Tanzania ilianzisha siku ya afya na lishe ya kijiji katika miaka ya 1980 ikilenga kuongeza ufuatiliaji wa lishe ukuzaji wa viwango vya vituo vha afya katika kutoa huduma kwa kuongeza elimu ya unyonyeshaji, chanjo, matumizi ya Oral Rehydrated Salt (ORS) na uanzishaji wa chakula cha nyongeza.

 Ameongeza kuwa tangu mwaka 2023 wadau tofauti nchini wameijumuisha siku ya afya na lishe ya kijiji au mtaa kama sehemu muhimu katika program zao ambazo zimeonekana kuwa nzuri katika kutoa huduma kamili za maendeleo ya awali ya mtoto pamoja na huduma za lishe katika ngazi ya jamii.

Wakichangia kwa nyakati tofauti Kelvin Gilo ambae ni mtendaji wa mtaa wa Igumamoyo kata ya Sangabuye na Asha Mahiza ambae ni Afisa elimu kata ya Nyakato wameshauri kutengwa kwa bajeti toshelezi kwa ajili ya  kufanikisha shughuli zote za lishe ikiwemo uelimishaji sambamba na mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayosimamia masuala ya lishe.

 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa