Home » » JAMII YATAKIWA KUACHA DHANA POTOFU DHIDI YA UNYONYESHAJI

JAMII YATAKIWA KUACHA DHANA POTOFU DHIDI YA UNYONYESHAJI

Jamii imetakiwa kuacha dhana potofu dhidi ya unyonyeshaji ili kuwafanya watoto kuwa na afya njema na kukua vizuri kimwili na kiakili.

Hayo yamebainishwa na mwakilishi wa mganga mkuu wa manispaa ya Ilemela Dkt. Barnabas G. Mwaikuju  wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani yaliyofanyika katika viwanja vya kituo cha Afya Buzuruga ambapo amekemea imani na fikra potofu zinazochangia kukwamisha unyonyeshaji wa watoto ikiwemo kuamini watoto wasiponyonya mama atabaki kuwa binti, kuwanywesha watoto maji badala ya kunyonya wakiamini kila mtoto anapolia anakuwa na kiu hivyo kushauri kuzingatia ushauri wa wataalam katika kunyonyesha watoto kwa ufasaha.

‘.. Kunyonyesha mtoto ni msingi bora wa ukuaji wake,huimarisha viungo na akili..' Alisema

Aidha Daktari Mwaikuju amewasisitiza wazazi na walezi kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma za afya pindi zinapojitokeza changamoto wakati wa unyonyeshaji badala ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji na watu wengine wasiokuwa na utaalamu.

Nae Bi. Pili Kasimu ambae ni mratibu wa lishe kwa manispaa ya Ilemela amewataka wa mama kuzingatia lishe za watoto ili kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo mdomo wazi, kichwa kikubwa pamoja na kutumia dawa za kuongeza damu na si kuzitupa.

Damarice Dawson ni muuguzi katika kituo cha Afya Buzuruga ambapo amewaonyesha wazazi waliohudhuria katika maadhimisho hayo namna bora ya kunyonyesha watoto pamoja na kuzingatia mkao, namna ya kuwabeba na kuwashika ili watoto waweze kunyonya kwa urahisi.

Anna Boniphace na Joanita Philipo ni wananchi kutoka mitaa ya Nyambiti na Buzuruga ambapo wameshukuru kwa elimu iliyotolewa huku wakiahidi kuizingatia na kuifanyia kazi ili watoto wao wakue vizuri pamoja na kuwaelimisha wananchi wengine.

Wiki ya maadhimisho ya unyonyeshaji maziwa ya mama hufanyika kila mwaka Agosti 1-7,  kwa mwaka huu imebebwa na kauli mbiu ya ‘Tatua changamoto, Saidia unyonyeshaji kwa watoto’ huku kwa ilemela ikiadhimishwa kwa kutoa elimu na kuhamasisha juu ya unyonyeshaji katika vituo vyote vya kutolea huduma na katika jamii kupitia maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIM).

 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa