Home » » MKANDARASI ASIMAMISHWA KUJENGA MAABARA

MKANDARASI ASIMAMISHWA KUJENGA MAABARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KAMPUNI ya UK General Services, imesimamishwa kuendelea na ujenzi wa maabara katika shule ya Sekondari ya Mbugani kutokana na kushindwa kukidhi vigezo.
Akizungumza jijini hapa jana, Mjumbe wa Kamati ya shule hiyo, Gaya Wandole, alisema kusimamishwa kwa kampuni hiyo kumetokana na kuomba fedha kabla ya hatua ya awali ya ujenzi wa msingi wa jengo hilo haujakamilika.
Alisema kampuni hiyo ilipewa dhamana ya ujenzi wa maabara ya vyumba vitatu vilivyopaswa kujengwa ndani ya wiki nane, lakini mkandarasi huyo hakufuata matakwa na kupeleka hati ya madai ya sh milioni 2.9.
Wandole, alisema baada ya kampuni hiyo kupeleka maombi ya fedha hizo kwa bodi ya shule na Kamati ya Maendeleo ya Kata, waliafikiana kuisimamisha kazi na kuweka mafundi wa kawaida ili kukamilisha ujenzi kabla ya Desemba.
“Oktoba 15 mwaka huu, tulikaa kikao kujadili namna tutakavyomlipa mkandarasi huyo, lakini hatukuafikiana na tukaamua kumsimamisha kazi, sababu zikiwa ni Jiji kutoa sh milioni mbili,” alisema Wandole.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Mbungani, Hassan Awadh, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema taarifa hizo hazina ukweli.
Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa kampuni hiyo ziligongwa mwamba, baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Uk General Services, iliingia mkataba na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Mbugani, kujenga vyumba sita vya maabara katika shule mbili za Mtoni na Mbugani Sekondari kwa gharama ya sh milioni 259.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa