Home » » CCM YATAKA WATU BINAFSI WASIPEWE TENDA

CCM YATAKA WATU BINAFSI WASIPEWE TENDA

na Sitta Tumma, Kwimba
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimemuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kurejesha mamlaka ya ugawaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo cha pamba kwa vyama vya ushirika nchini, badala ya kazi hiyo kufanywa na makampuni ya wafanyabiashara.
Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Ngudu, katika ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri Mkuu.
Mabina alisema ni vema mfumo wa usambazaji wa pembejeo za kilimo ukarejeshwa kwa vyama hivyo vya ushirika vyenye matawi hadi vijijini, kama ilivyokuwa enzi ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, suala la usambazaji wa pembejeo za kilimo CCM mkoa wa Mwanza inashauri lirejeshwe kwa vyama vya ushirika. Ukirejeshwa huko wananchi wetu watapata mbegu na dawa kwa wakati kuliko kazi inayofanywa na makampuni ya wafanyabiashara.
“Tunajua vyama hivi vya ushirika vina matawi kwa kila vijiji nchini. Pia vinafahamu mbegu bora ni ipi, na isiyo mbegu bora nayo ikoje. Na kazi hii ikirejeshwa huko, maana yake hata serikali itakuwa rahisi mno kuviwajibisha pale vinapoenda kinyume,” alisema mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mwanza.
“Ukimpa mtu kazi ya kusambaza mbegu wakati hajui ubora wake na utofauti wake kwamba mbegu hii ukiipanda muda huu utapata mavuno mengi, nahii ukiipanda miezi hii utapata mali nyingi hatuwezi kuwasaidia wananchi wetu kujikomboa na umaskini kupitia kilimo cha pamba,” alisema Mabina.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Pinda alisema serikali inathamini na kutambua umuhimu wa zao la pamba na kwamba mwaka jana makampuni mengi yanayonunua pamba duniani yalipata hasara kubwa, ikiwemo India.
“Serikali imelazimika kutazama upya namna ya kumuongezea mkulima wa pamba bei. Na hii inatokana na nchi nyingi duniani zinazonunua pamba kwa wingi uchumi wake kuporomoka...lakini serikali inaangalia namna gani tena ya kuwasaidia zaidi wananchi wetu; na ushauri kama huu wa Mabina ni mzuri sana,” alisema Pinda.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa