Home » » WAGOMBEA CCM WAJAWA HOFU MWANZA

WAGOMBEA CCM WAJAWA HOFU MWANZA

Na John Maduhu, Mwanza
WAKATI vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinatarajiwa kuanza leo, hofu imetanda miongoni mwa wagombea wa nafasi mbalimbali za chama hicho katika ngazi za wilaya na mkoa.

Hofu hiyo imetokana na kuwapo kwa makundi yanayotofautiana ndani ya chama hicho, huku kila kundi likijitahidi kujenga ngome yake kwa wafuasi wao kuhakikisha wanapitishwa katika vikao vya juu na hatimaye waweze kuwania nafasi walizoomba.

Vikao hivyo vinatarajiwa kuanza kwa sekretarieti ya chama hicho kuketi kupitia majina ya wagombea walioomba nafasi za Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), uenyekiti wa wilaya na mkoa.

Kikao hicho cha sekretarieti kitafuatiwa na kikao cha Kamati Kuu na baadhi ya waliokuwa wagombea wa nafasi mbalimbali, walioenguliwa katika vikao vya wilaya na mkoa kwa kupewa alama wanazozilalamikia tayari wamekata rufaa katika ngazi za juu za chama hicho.

Wanachama wa chama hicho waliojaziwa alama za chini wamekuwa wakilalamika kuwa, taratibu katika baadhi ya vikao zilikiukwa kutokana na misingi ya makundi pamoja na chuki binafsi na kuvitaka vikao hivyo kurejesha majina yao.

Aliyekuwa mgombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela, Richard Rukambura, tayari amewasilisha malalamiko yake katika vikao vya juu, kwa maelezo jina lake lilijaziwa alama za chini katika ngazi ya mkoa na kumuengua katika mapendekezo yake licha ya wilaya kumuona ana sifa.

“Nimeamua kukata rufaa kwa kuwasilisha malalamiko yangu kwa Kamati Kuu, kutokana na namna chuki zilivyotawala katika kutoa mapendekezo ngazi ya mkoa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza ndiye chanzo cha malalamiko ya wagombea wengi walioenguliwa kutokana na kukiyumbisha chama chetu.

“Kama suala ni tuhuma mbona Mwenyekiti wa CCM Mkoa ana tuhuma mbalimbali, zikiwa ni pamoja na kunyang’anya wananchi mashamba, lakini kwa mshangao wa wengi aliamua kujipendelea kwa kushawishi wajumbe kumjazia alama za juu ambazo hastahili.

“Ila sisi wengine tusio na sauti hatukupendekezwa hivyo Kamati Kuu inapaswa kutengua mapendekezo ya wagombea wa nafasi mbalimbali,” alisema Rukambura.

Naye, James Bwire, aliyekuwa akiwania nafasi ya ujumbe wa NEC Wilaya ya Nyamagana, alisema ameamua kukata rufaa kutokana na jina lake kuenguliwa katika ngazi ya mkoa, licha ya kupewa alama za juu katika vikao vya chini.

Mmoja wa wabunge wa zamani wa chama hicho aliyepewa alama za chini kuanzia ngazi za wilaya na mkoa, alisema alipewa alama hizo kutokana na fitina ya kundi moja linaloongozwa na mmoja wa wabunge pamoja na viongozi wa wilaya na mkoa kwa maslahi binafsi.

“Nimekuwa mbunge kwa miaka 10, pia nimeshika nyadhifa mbalimbali, leo hii ninapewa alama D kwa kosa lipi, CCM isipokuwa makini kupitia vikao vyake vya ngazi za juu, itakwenda kuangamia kwa kuwa sasa inaongozwa kwa chuki.

“Kuna wagombea ambao wana uwezo mkubwa walienguliwa katika ngazi za wilaya, pia kuna wagombea ambao wana uwezo mdogo na hawana uzoefu ndani ya chama, ila kwa kuwa wako kwa maslahi ya viongozi wamerejeshwa kwa kupendekezwa, vikao vya mkoa si msahafu ndio maana suala hili la madudu ya CCM mkoa tumeamua kulifikisha katika vikao vya juu,” alisema kwa sharti la kutotajwa jina.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa