Home » » DK. CHEGENI: MAKUNDI YAMEIDHOOFISHA CCM

DK. CHEGENI: MAKUNDI YAMEIDHOOFISHA CCM


Na John Maduhu, Mwanza
MBUNGE wa zamani wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, amesema makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekidhoofisha kwa kiasi kikubwa na kitaanguka katika uchaguzi mkuu ujao endapo wanachama hawatayaona mabadiliko ya kweli katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Kauli hiyo aliitoa mapema wiki hii, wakati akirejesha fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Wilaya ya Busega katika ofisi za chama hicho.

Alisema CCM imekuwa ikikabiliwa na adui mkubwa, makundi, anayetishia uhai wa chama hicho na kuwataka wanachama kuhakikisha wanatumia fursa ya uchaguzi kuwaweka pembeni viongozi ambao ni vinara wa makundi.

“Katika siasa kuna kushinda na kushindwa, wengine wakishindwa wanaingia msituni na kuanza vurugu kwa lengo la kukivuruga chama, hali hii ni mbaya katika siasa za ushindani, lazima tukubali kushinda na kushindwa na tuache kujenga kambi za kukomoana ndani ya chama,” alisema Dk. Chegeni.

Aidha, aliwapongeza vijana wa chama hicho kutokana na uamuzi wao wa kumchukulia fomu za kuwania nafasi ya NEC Wilaya ya Busega na kuahidi kuwa atawatumikia kwa nguvu zake na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoanza wakati akiwa mbunge.

Kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mwanza kimezidi kushika kasi, baada ya kuwapo kwa wagombea 21 waliojitokeza.

Katika hatua nyingine, aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali, Mashimba Mashimba, alisema ameamua kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kukirejesha chama hicho katika mikono ya wakulima na wafanyakazi.

Alisema matumizi ya fedha katika kusaka uongozi ndani ya CCM yamewafanya wanachama wa kawaida ambao ni wakulima na wafanyakazi kukaa pembeni na kushindwa kuwania nafasi kutokana na kutokuwa na nguvu ya fedha.

Alisema akifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho atahakikisha matumizi ya fedha katika kusaka uongozi yanakomeshwa.

Kwa upande wake, Evance Mabugo (34), amejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza na kueleza kuwa ameamua kujitoa mhanga wa kupambana na wagombea wakongwe ndani ya chama hicho.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa