Home » » JAMII YAASWA KUTOFUJA MALI ZA YATIMA

JAMII YAASWA KUTOFUJA MALI ZA YATIMA


Na John Maduhu, Mwanza
JAMII imetakiwa kutojitwalia mali za watu wanaowatunza wakiwamo wajane na yatima na badala yake, wanatakiwa kuzitunza na kuhakikisha mali hizo zinakuwa endelevu kwa ajili ya walengwa.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mlezi wa Jamii ya Kiislamu ya wanachuo wanaosoma Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) jijini Mwanza, Altaf Hiran Mansoor wakati akifunga mkutano wa kuendeleza Qur’an na Sunna.

Kwa mujibu wa maandiko ya dini ni marufuku kwa wale waliopewa dhamana ya kuwaangalia wanyonge, yatima na wajane kutojitwalia mali za wanaowatunza.

“Maandishi ya dini yanawaonya watu au viongozi wenye kupenda rushwa dhidi ya kushiriki dhuluma dhidi ya mali za wanyonge ,” alisema Altaf.

Mlezi huyo wa wanafunzi wa kiislamu pia alikipongeza chuo hicho kutokana na namna kilivyotoa nafasi kwa wanachuo hao kuabudu licha ya chuo hicho kuwa chuo cha Kikristu.

Altaf alisema kuwa, akiwa mlezi wa wanachuo hao atahakikisha anashirikiana nao katika kuhakikisha vijana hao wanakuwa na malezi bora na kutatua matatizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwakabili.

Mlezi huyo pia aliipongeza Jumuiya ya Kuendeleza Qur'an na Sunna kutokana na kuwakutanisha viongozi wa dini wakiwamo masheikh kujadili mambo mbalimbali ya kijamii.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa