SOKO LA MWALONI LATOA AJIRA KWA VIJANA
BAADHI ya vijana waliofanikiwa kupata ajira katika soko la Kimataifa la Mwaloni soko linaloelezwa kuajiri zaidi ya vijana 600 katika shughuli mbalimbali,hapa anaonekana wakichakata vichwa vya samaki (MAPANKI) vilivyokwishaondolewa minofu kwenye viwanda vya kuchakata samaki ambapo baadaye huvikausha na kisha kuuza kwa wananchi wa kawaida ndani na nje ya nchi.
(Picha na David Azaria)
Na David Azaria,SAUT-Mwanza
SOKO la Samaki la Mwaloni Katika Jiji la Mwanza limefanikiwa kutoa Ajira kwa zaidi ya Vijana 600 ambao wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo ubebaji wa mizigo na hivyo kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.
Aidha Soko hilo pia limetoa ajira kwa wanawake wajane pamoja na wale walioachwa ama kutelekezwa na waume zao ambao wamekuwa wakifika katika soko hilo na kufanya shughuli na hivyo kujipatia fedha za kuweza kusaidia familia zao kwa malazi chakula pamoja na mavazi.
Akizungumza na mwandishi wa Geita yetu aliyeko katika mafunzo ya Habari za uchunguzi katika habari za biashara na Uchumi kwenye mahojiano maalum juu ya manufaa ya soko hilo tangu kujengwa kwake mwaka 2005, Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko hilo Christopher Wankyo, alisema kuanzishwa kwa soko hilo kumesaidia kutengeneza ajira nyingi kwa vijana pamoja na akina mama ambao kama soko lisingekuwepo wangekuwa wakitaabika mitaani.
Alisema zaidi ya watu 1000 wanajihusisha na shughuli za kibiashara katika soko hilo kila siku, huku akibainisha kuwa robo tatu ya watu ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35 ambao wamekuwa wakijihusisha hasa na shughuli za upakuaji na upakiaji pamoja na usombaji wa mizigo mbalimbali.
“Kazi nyingi katika soko hili ni za kutumia nguvu na ndiyo maana unaona vijana ndio wengi ndani ya soko hili kwa sababu inaaminika kwamba wao wana nguvu, kwa hiyo kila siku soko linatengeneza ajira kwa zaidi ya vijana 600 ambao hawa wanapata fedha zao taslimu kila siku baada ya kazi……’’ anasema Mwenyekiti huyo na Kuongeza.
“Lakini bado pia kuna akina mama hapa ambao wengi wao ni wajane nao wanafanya biashara za aina mbalimbali ndani ya soko ikiwa ni pamoja na kuuza mbogamboga na dagaa, pamoja na samaki na hivyo kujipatia fedha za kujikimu kimaisha…..’’.
Wakizungumza Geita yetu baadhi ya vijana wanaojishughulisha na biashara pamoja na shughuli mbalimbali ndani ya soko hilo ikiwemo upakuaji na upakiaji wa mizigo Bandarini, walisema uwepo wa soko hilo umewapatia ajira za kudumu ambazo zinawafanya kumudu gharama za maisha ya kila siku.
“Kwa mfano mimi hapa kazi yangu kila siku ni kukatakata vichwa vya samaki vinavyotoka kiwandani kwa ajili ya kuandaliwa kabla ya kukaushwa na kuepelekwa kwa walaji, lakini ninapotoka hapa nakuwa na fedha yangu taslimu ambayo ni mali yangu kwa kazi nilizofanya siku nzima….’’ Alisema Mmoja wa vijana hao Enos Lucas na kuongeza:
“Kama mzigo unakuwa mkubwa sana basi kwa siku naondoka na sh. 40,000 au sh.50,000 pamoja na kwamba kazi ni ngumu lakini fedha inayopatikana ni nzuri na inasaidia kuendesha maisha ya kila siku kwa sababu tuna familia ambazo zinatutegemea’’.
Kwa upande wao John Elias, Zakayo Kingi na Mabula George wanasema uwepo wa soko hilo umewafanya kupata ajira kwani fedha wanazozipata zimekuwa zikiwasaidia kuendesha maisha yao ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wao pamoja na wadogo zao.
“Kama hili soko lisingekuwepo sijui sasa hivi ingekuwaje, vijana tuko wengi sana humu ndani na tunapata fedha za kutosha kabisa, kama mtu unajituma huwezi kukosa sh.20, 000 kwa siku ama zaidi, kwa sababu ukitoka hapa unakuwa umechoka unakwenda nyumbani kupumzika hakuna yale mambo ya kujirusha mitaani, soko lisingekuwepo basi hali ingekuwa ni tete huko mitaani, ingekuwa ni wizi mtindo mmoja…..’’ alisema Mabula.
Kwa upande wao baadhi ya wakina mama ambao nao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo ubebaji wa mizigo katioka soko hilo, walisema uwepo wa soko hilo umewafanya kujishughulisha na hivyo kujipatia fedha za kuendesha maisha ya familia zao bila kutegemea wanaume.
“Kila siku nakuja hapa kazi yangu kubwa ni kusomba vichwa vya samaki na kuleta kwa hawa wakataji, ninapotoka jioni natoka na sh.30,000 au zaidi ambazo zinatosha kabisa kuwalisha watoto wangu watatu ambao ninaoishi nao nyumbani kwangu Igogo nilipopanga, ndivyo maisha yanavyokwenda…’’ alisema Getruda Joram ambaye ni Mama Mjane.
Soko la Mwaloni lilijengwa na Halmashauri ya jiji la Mwanza na kuanza kufanya kazi mwaka 2005, ambapo soko hilo limekuwa likizalisha samaki aina ya Sangara wakavu na wale wa Kubanikwa pamoja na Dagaa ambao soko lao kubwa liko nje ya Nchi ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo,Msumbiji,Burundi na Rwanda.
Mwandishi wa habari hii anachukuwa mafunzo maalum ya Habari za Uchunguzi katika Biashara na Uchumi katika Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Jijini Mwanza,na Habari hii ni moja ya mazao ya Mafunzo anayoendelea nayo katika Chuo hicho.
0 comments:
Post a Comment