Na John Maduhu, Mwanza
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, mwishoni mwa wiki alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Dhahama hiyo ilitokea wakati wa kikao cha ndani baina ya Mabina na madiwani hao, ambapo hatua hiyo ilisababisha kuvunjika kwa kikao cha Baraza la Madiwani.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Mabina kudaiwa kuwatuhumu baadhi ya madiwani hao, kwamba wamehongwa fedha ili kumlinda Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Benard Polly.
Mabina alitoa matamshi hayo katika ukumbi wa CCM wa wilaya na kuwachefua madiwani hao. Katika kikao hicho Mabina aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mariamu Rugaila.
Wajumbe wengine waliokuwapo katika msafara huo ni pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Magunga na wajumbe wawili wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa.
Katika mkutano huo mwenyekiti huyo aliwatuhumu madiwani hao kuwa, wameshindwa kumwajibisha mwenyekiti wa halmashauri hiyo kutokana na wao kuhongwa Sh milioni saba.
Kufuatia kauli hiyo madiwani hao walimtaka Mabina kuthibitisha kauli yake na kutoa ushahidi kwa kuwa tuhuma alizozitoa dhidi yao ni nzito na hazikupaswa kutolewa katika kikao hicho.
"Mheshimiwa mwenyekiti tuhuma hizo ni nzito dhidi yetu, tuhongwe fedha kwa ajili ya nini hasa? wewe mwenyewe mbona umekuwa ukituhumiwa kwa rushwa tena katika vikao na hujachukua hatua, tunaomba utuombe radhi vinginevyo tutakuchukulia hatua", alisema diwani mmoja, huku wengine wakizomea.
"Hakika baada ya kauli hiyo ya Mwenyekiti dhidi ya madiwani hali ya hewa ilichafuka na kila diwani alitoa kauli nzito dhidi ya Mabina.
“Madiwani walimzomea kwani alitudhalilisha suala la mwenyekiti wetu kwa mujibu wa msimamo wa baraza la madiwani ni kuviachia vyombo vya dola vifanye kazi bila kuingiliwa na kama ana kosa basi afikishwe mahakamani sio kutumia ngao ya CCM kumwadhibu kutokana na chuki binafsi", alisema diwani mwingine.
Kutokana na zomea zomea hizo Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mariamu Rugaila aliomba kikao hicho kifungwe, ili kuepusha kutokea kwa vurugu zaidi hali ambayo inaweza kuhatarisha hali ya usalama.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment