Home » » Waandishi wa habari wafundwa mbinu za kuandika habari za uchunguzi katika biashara na uchumi

Waandishi wa habari wafundwa mbinu za kuandika habari za uchunguzi katika biashara na uchumi





HAWA ni baadhi ya Waandishi wa habari wanaochukua mafunzo ya Habari za uchunguzi za Biashara na Uchumi katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Jijini Mwanza (Picha na David Azaria)


Na David Azaria, SAUT-Mwanza yetu 
WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kujikita  katika uandishi wa habari za Biashara na Uchumi ili kuibua fursa za kibiashara hususani mipakani ili kuwafanya Watanzania kuelewa mazingira ya kibiashara  vizuri na kuyatumia. 
Ushauri huo umetolewa na Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Mtakatifu Augustin  kilichoko jijini Mwanza Padri Charles Kitima hivi karibuni wakati akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi juu ya biashara na uchumi yatakayodumu kwa mwaka mmoja kwa awamu nne tofauti yanayofanyika katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). 
Mafunzo hayo yanawashirikisha jumla ya waandishi wa habari 30 kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari nchini, ambao walipatikana kufuatia mchujo kutoka miongoni mwa waandishi wa habari zaidi ya 60 waliotuma maombi yao kuomba kujifunza mafunzo hayo. 
Padri Kitima alisema kuwa sio kila mtu anaweza kuelezea habari inayoifaa  jamii bali waandishi pekee ndio kiungo muhimu hapa nchini na duniani kote ambao wanaweza kutoa maelezo mazuri kwa kuonyesha changamoto na mafaniko mwishowe fursa zilizopo ziweze kitumika ipasavyo. 
“Waandishi mkichambua vizuri kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania kuanzia ngazi za vijijini mpaka taifa wananchi watajifunza  na kuzitambua fursa zilizopo na kuzitumia kisha wataepukana na dhana ya Rais wa nchi atuletee pesa na wakati wana uwezo wa kutumia fura hizo kujikomboa na lindi la umaskini na kukuza uchumi wao wenyewe”alisema Padri Kitima na kuongeza. 
“Vyuo vikuu vyote vinavyojihusisha na kufundisha masomo ya uandishi wa habari havikuwahi kufundisha somo la uandishi wa habari za biashara na uchumi, kwa hiyo ni changamoto ambayo inatukabili, ni muhimu kwenu kutumia mafunzo haya kuhakikisha mnaibua mianya na fursa za kiuchumi kwa kuandika habari za uchunguzi zinazohusu uchumi ili vikwazo viondolewe…..’’. 
Alisema kwa upande wake anaamini wananchi wakizifahamu fursa zilizopo na wakazitumia ipasavyo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika maisha yao, tofauti na ilivyo sasa ambapo kila mmoja anamlilia rais kwamba ndiye chanzo cha mambo yote hususani suala zima la mfumuko wa bei hali iliyosababisha kupanda kwa gharama za maisha. 
“Kwa mfano angalia nchi za wenzetu wao wanafanya biashara masaa 24 lakini Tanzania tunafunga benki saa kumi alasiri wakati muda huo Marekani ni saa nne za asubuhi tunadai kuwa hayo mambo ya kufanya biashara usiku na mchana ili kukuza uchumi ni ya nchi zilizoendelea….’’ Alisema Kitima.
Alibainisha kuwa endapo nchi inahitaji kubadilika na kuingia katika rekodi za miongoni mwa nchi zenye uchumi mzuri na unaoheshimika ni lazima waandishi wa habari wajitume na kuandika habari zinazohusu uchumi na kuwafumbua macho Watanzania katika suala zima la kutumia fursa zilizopo hususani sekta ya utalii ambapo aliishauri Serikali kuwa asilimia 90 ya uwekezaji katika sekta ya utalii  ni vyema ikamilikiwa na wazawa ndipo uchumi utaweza kupanda na kukua kwa kasi. 




0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa