na Sitta Tumma, Mwanza
KITENDO cha kuondolewa kwa magari mawili ya kubeba wagonjwa katika vituo vya afya vya Nassa na Lukungu, Jimbo la Busega Mkoa mpya wa Simiyu, limechukua sura mpya baada ya wananchi wa wilaya na jimbo hilo kudai kwamba magari hayo yamehujumiwa na baadhi ya wanasiasa.
Wamesema, hujuma hizo ambazo wamezifananisha na za ‘kishetani’ zimekuwa zikifanywa na baadhi ya wanasiasa waliomo madarakani kwa sasa kwa kuyaharibu magari hayo, yaliyotolewa kwa msaada na mbunge wa zamani wa Busega, Dk. Raphael Masunga Chegeni (CCM), wakati wa uongozi wake.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa nyakati tofauti jimboni humo, baadhi ya wakazi wa wilaya na jimbo hilo walidai magari hayo yameondolewa katika vituo hivyo yakiwa mazima.
“Hujuma hizo zimelenga kuharibu miradi iliyotolewa na Dk. Chegeni wakati wa uongozi wake, jambo lililosababisha kero ya wananchi kukosa huduma muhimu ya magari ya kubeba wagonjwa,” alisema mmoja wa wananchi.
Kwa mujibu wa wananchi hao, magari hayo yaliondolewa katika vituo hivyo na kupelekwa katika yadi ya Idara ya Ujenzi katika Halmashauri ya Magu mkoani Mwanza, baada ya kile kinachodaiwa kuhujumiwa vipuri vyake na wanasiasa hao baada ya kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2010.
Wakizungumza kwa jazba, wananchi hao walishangazwa na kitendo cha Mbunge wa sasa wa jimbo hilo la Busega, Dk. Titus Kamani (CCM), kuhoji bungeni kuhusu magari hayo yalipo, na kudai kwamba mbunge huyo anafahamu fika hujuma hiyo na yalipo kwa sasa.
Walisema kuwa mbunge huyo alipaswa aulize swali hilo kwenye vikao vya madiwani Magu, na si bungeni.
Wananchi hao wameitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wote walioshiriki kuhujumu magari hayo ya wagonjwa, na kutaka yarudishwe ili yaendelee kutoa huduma
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment