Home » » Bil. 2/- kunufaisha wakulima Kanda ya Ziwa

Bil. 2/- kunufaisha wakulima Kanda ya Ziwa


na Bigambo Jeje, Mwanza
MRADI wa uwekezaji katika sekta ya kilimo wilayani (DASIP) unaotekelezwa katika mikoa saba ya Kanda ya Ziwa umetenga sh. bilioni 2.1 kwa ajili ya kuvijengea uwezo vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) vya wakulima na wafugaji vijijini ikiwa ni hatua ya kuwainua kutoka katika dimbwi la umaskini.
Kaimu Mratibu wa DASIP Jovin Kangimba alisema fedha hizo zitakazoanza kutumika katika mwaka huu wa fedha wa 2012/13 zitatumika katika andiko la mradi wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji katika vikundi na vyama vyao vya ujasiriamali.
Akielezea lengo la mradi huo alisema ni kuzifikia SACCOS 84 sanjari na kuzisaidia na kuziwezesha ili ziweze kujiendesha na kufikia malengo zilizojiwekea ikiwa ni pamoja na kupata sifa za kukopesheka na taasisi mbalimbali za fedha zikiwamo benki za hapa nchini.
Katika hilo alisema mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo vijijini umeamua kununua na kusambaza pikipiki 56 zenye thamani ya sh milioni 250 kwenda katika wilaya 28 kwa lengo la kuwasaidia maofisa wa DASIP kuwafikia wakulima na kuziimarisha SACCOS hizo.
Kangimba alisema vyama vya kuweka na kukopa vitakavyonufaika na msaada huo ni vile vilivyoanzishwa chini ya DASIP ilipoanza utekelezaji wa mradi wake katika wilaya 28 za mikoa saba ambayo ni Mara, Kagera, Shinyanga, Kigoma, Mwanza, Geita na Simiyu.
Mradi huo unatekelezwa kati ya mfadhili mkuu Benki ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa