Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMPUNI ya Free Media imetambulisha gazeti la Tanzania Daima Kanda ya Ziwa.
Hafla hiyo ilifanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki katika Hoteli
ya Villa Park na kudhaminiwa na kampuni inayotengeneza kinywaji cha bia
aina ya Windhoek.
Mikoa ya Kanda ya Ziwa itakayonufaika na mpango huo ni Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita, Kagera, Simiyu na Kigoma.
Utambulisho huo umelenga kuimarisha usambazaji na uuzaji wa gazeti
hilo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kufika kwa wakati kwa wananchi.
Akizungumza katika utambulisho huo, Mhariri Mtendaji wa Free Media,
Ansbert Ngurumo, aliwapongeza Watanzania kwa kuwa wasomaji wazuri wa
Tanzania Daima.
Alisema kuanza kuchapishwa kwa gazeti la Tanzania Daima jijini hapa
ni utaratibu uliolenga kuleta mageuzi katika tasnia ya habari na
kuwafikia wananchi mapema kuliko ilivyokuwa hapo awali.
“Tanzania Daima imeanzishwa kwa mrengo wa kisiasa. Huu ndio ukweli
wake. Lakini kutokana na ubora wa habari zake zinazozingatia taaluma na
weledi wa masuala ya habari katika kupeleka ujumbe kwa jamii, wananchi
wanalipenda sana gazeti hili.
“Na wakati tukijivunia haya yote, sisi ambao ni watendaji wakuu wa
gazeti hili, maisha yetu yapo hatarini…na mkisikia leo tumekufa si
ajabu. Na bora tufe tukipigania haki kuliko kukanyaga haki,” alisema
Mhariri Ngurumo na kuongeza:
“Nikiwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima na Sayari,
nimepokea ushauri, maombi na mambo yote mliyotukosoa. Wengine wameguswa
na Kolamu yangu ya Maswali Magumu, kimsingi Maswali Magumu ninayatungia
kitabu kitakachoifikia jamii baada ya kukamilika kwake. Karibuni sana
sote tuijenge Tanzania Daima kwa masilahi ya taifa na wananchi wake
wote.”
Baadhi ya wachuuzi wa magazeti jijini Mwanza wanasema gazeti la
Tanzania Daima Jumatano na Jumapili, ndiyo yanayouzwa kwa wingi kutokana
na habari zake nyingi kuwa za uchambuzi na makala zinazosisimua na
kukonga nyoyo za Watanzania.
Baadhi ya wadau waliipongeza Tanzania Daima kwa uhodari wake wa kufichua maovu yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali.
Kwa upande wao, Mhariri wa Tanzania Daima Jumatano, Edson Kamukara
pamoja na Meneja Matangazo wa Free Media, Marcus Mtinga, walisema
kampuni hiyo imejipanga vizuri kuhakikisha inaboresha zaidi huduma zake.
“Si siri, Tanzania Daima tumejipanga vizuri sana kuboresha huduma
zetu kulingana na mahitaji ya wananchi. Tutaendelea kusema ukweli daima,
na hatutaogopa chochote wala vitisho. Tunayakaribisha mashirika, asasi,
kampuni na taasisi zote za umma na zile za watu binafsi kuleta
matangazo kwetu,” alisema Kamukara.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment