MBUNGE wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (CHADEMA),
amemshambulia Meya wa jiji hilo, Stanslaus Mabula (CCM), akimuita ni
mzigo aliyesababisha jiji kuwa na ukata mkubwa wa fedha za maendeleo.
Alisema pamoja na jiji kukumbwa na ukata huo, Mabula ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Mkolani, amesababisha jiji hilo kuwa chafu na kwamba
amekuwa akiwakashifu na kuwabeza wafanyabiashara wadogo (Machinga).
Wenje alitoa shutuma hizo juzi wakati akihutubia mamia ya wakazi wa
Jiji la Mwanza, katika mkutano wa hadhara wa Operesheni M4C Pamoja
Daima, uliofanyika viwanja vya Furahisha.
Huku akimuita Mabula Meya wa ‘Kichina’, Wenje alisema kwa sasa
halmashauri hiyo imekumbwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha, huku
viongozi wake wakilalamikia hali hiyo.
“Huyu Meya wa Kichina, analalamika eti jiji halina hela. Wakati
anatakiwa na miwani yake afanye kazi kwa ubunifu ili vyanzo vya mapato
viongezeke, amebaki akilialia.
“Wakati CHADEMA ilipoongoza jiji hilo kabla ya kuhujumiwa na CCM,
jiji lilikuwa na fedha nyingi kutokana na vyanzo vyake, na lilikuwa safi
nchi nzima,” alisema.
Kwa mujibu wa Wenje, kwa sasa Mabula analalamika kuwa jiji ni chafu kwa sababu mbunge aliruhusu kuwepo machinga mjini.
“Kwani machinga ni uchafu? Mama ntilie ni uchafu?” alihoji Wenje kisha kushangiliwa.
Akizungumzia ugumu wa maisha unaowakabili wananchi kwa sasa, alisema
Bunge lijalo wabunge wa CHADEMA watapambana bungeni kuhakikisha bei ya
umeme inashuka kuliko ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa Wenje, Watanzania wategemee kuona harakati za wabunge
wa CHADEMA wakipigania maendeleo ya wananchi, na kwamba wapo tayari
kupigwa ngwara zaidi ya ilivyotokea kwa Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’.
“Bei ya umeme imepanda, chumvi, sukari, sabuni na kila kitu.
Wamepitisha bei ya umeme sisi tukiwa nje ya Bunge kwenye likizo.
Tunasema tukirudi kwenye Bunge haki ya mama mpaka kieleweke, kama
mlivyoona wakimnyanyua Sugu, tupo tayari watunyanyue mara 10 ya Sugu,”
alisema.
Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA), alimtuhumu Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo, kwa madai kwamba amekuwa
akikwamisha maendeleo ya wananchi wa Ilemela.
Kiwia alieleza kwamba kiongozi huyo amekuwa chanzo kikubwa cha
kukwamisha maendeleo ya wananchi na alimtaka kubadilika mara moja.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment