Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa
Jiji la Mwanza juzi jioni lilitikisika kiasi cha baadhi ya shughuli kusimama kwa muda wa saa moja na nusu, kufuatia umati mkubwa wa wafuasi wa Chadema kutanda barabarani wakimsindikiza Dk. Slaa, baada ya kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara na kuhitimisha ziara yake jijini humo uliofanyika uwanja wa Furahisha.
Wafuasi hao waliamua kumsindikiza Dk. Slaa huku wakiimba nyimbo mbalimbali, na wengine wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti tofauti na wengine wakiwa vifua wazi na kupanda juu ya magari wakishangilia na kucheza.
Hali hiyo iliwalazimu wakazi wa jiji hilo kusimamisha shughuli zao na kusimama kando ya barabara na wengine kwenye mapaa ya nyumba huku wakishangaa ushangiliaji uliokuwa ukifanywa na wafuasi hao.
Daladala, pikipiki pamoja na watumia barabara za Nyerere, Makongoro walilazimika kusitisha shughuli zao kuanzia majira ya saa 12 jioni hadi saa 1: 30 usiku wafuasi hao walipomaliza kupita.
Ingawa umati huo ulizingira barabara hizo, lakini hakuna tukio lolote baya la kuvunja amani na utulivu lililotokea.
Kabla Dk. Slaa kuwasili katika uwanja wa Furahisha uliopo wilayani Ilemela kwa ajili ya kuhutubia, umati wa watu ulikuwa umeshafurika huku shamrashamra zikiendelea na mabango yenye jumbe mbalimbali yakipeperushwa.
Baadhi ya mabango hayo yalikuwa na ujumbe “Chadema hatutaki mamluki kwetu ni mwiko” na “Karibu Dk. Slaa.”
Majira ya saa 11 jioni Dk. Slaa aliwasili uwanjani hapo kwa helikopta na baada ya kupokelewa alikaribishwa kwa ajili ya kuwahutubia wananchi.
Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema wakati umefika sasa kwa Tanzania kufanya maamuzi magumu ya kuvunja mikataba yote ya kupeleka bidhaa ghafi nje ya nchi na badala yake kuanzisha viwanda vya ndani kwa ajili ya kutoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi.
Dk. Slaa aliongeza kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini imeshindwa kuzitumia na badala yake zinapelekwa kufaidisha watu wa nje kwa sababu ya kukosa viwanda huku akizitaja baadhi kuwa ni dhahabu, gesi, magogo na mazao ya kilimo ambazo alisema zingekuwa mkombozi wa uchumi wa Tanzania endapo viwanda vingekuwapo.
Alisema bidhaa hizo badala ya kuleta faida kwa nchi, zinayanufaisha mataifa mengine yenye viwanda na kwamba yanatumia gharama ndogo kutengeneza bidhaa na kuziuza kwa bei kubwa.
“Magogo, pamba, dhahabu ni mali yetu, lakini vinachukuliwa na kupelekwa nje kutengeneza cheni, vifungo, na kutuuzia kwa bei kubwa, mpaka lini tutategemea bidhaa za nje, kila bidhaa unayoina ni ile iliyotengenezwa China na sisi tutatengeneza za kwetu lini?” alihoji.
Aliongeza kuwa Chadema kikiingia madarakani ni lazima kipige marufuku usafirishaji wa dhahabu ghafi na mali nyingine ghafi nje ya nchi.
MBOWE ATIKISA MAILI MOJA
Shughuli za biashara zikiwamo za mikononi na za madukani katika eneo la Maili Moja, wilayani Kibaha mkoa wa Pwani juzi jioni zilisimama kwa zaidi ya saa moja baada ya wafanyabiashara na watu wengine kukimbilia katika viwanja vya Maili Moja kumsikiliza Mwenyekiti wa Chadema, Freman Mbowe.
Mbowe aliwasili katika viwanja hivyo juzi majira ya saa 11:00 jioni akitokea wilayani Kisarawe akitumia helikopta na baada ya kuingia eneo hilo makundi ya watu yalikuwa yakipigana vikumdo kuelekea eneo la mkutano na kuacha shughuli zao.
Umati ulijikusanya katika karibu na eneo la mkutano na kuwalazimisha walinzi wa chama hicho kuwadhibiti wananchi hao ili Mbowe aweze kupita kutoka katika helikopta na kuhutubia.
Kabla Mbowe hajaanza kuzungumza, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, aliwaeleza wananchi wa Kibaha kuwa chama hicho tayari imemtumia ujumbe Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kumueleza kwamba wananchi sasa wanataka mikataba ya ujenzi iwe wazi kwani wamechoshwa na mikataba isiyoeleweka ambayo imekuwa ikichangia wakandarasi wazembe na wasio na utaaalamu wa kutosha wa shughuli za ujenzi kupewa zabuni.
Naye Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Profesa Abdallah Safari, alisisitiza kuwa chama hicho siyo chama cha udini wala ukabila kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai kwa kutumia hoja hiyo kwa lengo la kuvuruga mashabiki na wanachama wa Chadema baada ya kuona chama hicho kinaimarika kwa kasi kubwa.
Profesa Safari alisema kuwa chama hicho kinafanya mambo yake kwa uwazi na ndiyo maana akitokea mwanachama ama kiongozi wake bila kujali nafasi aliyonayo akiisaliti, anawajibishwa kwa kushirikisha kamati zake zote husika na siyo kutumia mabavu ama mtu mmoja kufanya maamuzi pekee.
Akiwahutubia wananchi, Mbowe aliwataka wanachama na mashabiki wa Chadema nchini wawe kitu kimoja na watumie muda wao mwingi kuhamasishana kukijenga chama kwa maslahi ya Taifa.
Pia Mbowe alisisitiza kuwa lengo la chama hicho la kukusanya wanachama wengi zaidi linaendelea vizuri katika mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi, Morogoro na Mtwara.
Kuhusu Katiba mpya, Mbowe alisisitiza kuwa Chadema itahakikisha inapigania mawazo ya wananchi yabaki kama walivyoyapendekeza kwenye rasimu ya katiba.
Alisema maoni yaliyomo ni mawazo walioyatoa Watanzania wakati wa ukusanyaji maoni na siyo mawazo ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Joseph Warioba, kama baadhi ya wana siasa wanavyowadanganya wananchi.
Katika mkutano huo, wanachama watatu wa CCM wakiwamo viongozi wawili mjini Kibaha walirudisha kadi zao na kujinga na Chadema huku wakitaja sababu mbalimbali zilizowalazimisha kukihama chama tawala kuwa wamechoshwa na ufisadi uliopo na pia wamegundua CCM hakina dhamira ya ukweli ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
Viongozi waliokihama CCM na nafasi zao katika mabano ni Hafidh Muthihiri (mjumbe wa mkutano mkuu CCM Kibaha) na Joseph Chakwale (mjumbe kamati ya utekelezaji Kibaha).
Mwanachama mwingine aliyehamia Chadema ni Dk. Rose Mkonyi ambaye aliwahi kugombea ubunge jimbo la Kibaha Mjini kwa tiketi ya CCM, lakini alishika nafasi ya tatu katika kura za maoni baada ya kutanguliwa na Dk. Zainab Gama na Silvesrty Koka.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment