MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dk. Raphael Chegeni,
ameitaka kampuni ya uchimbaji madini katika mgodi wa Ngasamo wilayani
Busega, Simiyu kufuata sheria za nchi kwa kuwalipa fidia wananchi
wanaopisha mgodi huo.
Dk. Chegeni alitoa kauli hiyo juzi wakati alipokuwa akijibu maswali
ya baadhi ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya
Ngasamo, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM.
Baadhi ya wananchi walihoji sababu za wao kuondolewa katika maeneo
yao bila kulipwa fidia, jambo lililoonekana kumshitua Dk. Chegeni.
Alisema mwekezaji yeyote lazima ahakikishe anafuata taratibu na sheria za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Nimesikitika kusikia hampewi haki zenu. Nataka kila mtu anayetakiwa
apishe eneo hilo alipwe fidia yake. Na mwekezaji naye lazima afuate na
kuzingatia sheria katika hili,” alisisitiza.
Kuhusu utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini na majisafi ya
kunywa, alisema wakati akiwa mbunge wa Busega, alipigania miradi hiyo
na mingineyo, jambo ambalo serikali iliiweka kwenye mipango ya
utekelezwaji, na sasa imeshaanza kutekelezwa.
Alisema kwa sasa umeme wa vijijini (REA), umeshaanza kusambazwa
katika baadhi ya vijiji vya jimbo hilo, huku mradi mkubwa wa maji ya
Ziwa Victoria ukiwa katika utekelezaji, na tenki kubwa la maji
litajengwa maeneo ya Ngasamo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment