JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Aishieri
Sumari, amesema kesi nyingi za makosa ya jinai zimekuwa zikichelewa
kutolewa uamuzi kutokana na baadhi ya maofisa upelelezi kutokuwa na
utaalamu wa kutosha.
Jaji Sumari alitoa kauli hiyo jijini Mwanza jana kwenye maadhimisho
ya Siku ya Sheria yaliyofanyika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya
Mwanza jijini hapa.
Alisema kesi nyingi za makosa ya jinai zimekuwa zikichelewa kutolewa
hukumu na hiyo inatokana na kuwepo kwa wapelelezi wasiokuwa na utaalamu
wa kutosha.
Alisema ipo haja kwa serikali kuwapiga msasa kwa kuwasomesha zaidi
maofisa upelelezi, kwani hakuna sababu ya mtuhumiwa kukaa mahabusu
miaka mitano hadi sita bila upelelezi kukamilika.
“Kesi nyingi za jinai zinachelewa kutolewa hukumu kutokana na baadhi
ya wapelelezi ni wabovu na wanachelewa kukamilisha kazi zao kwa wakati.
“Naiomba serikali iwapige msasa maofisa upelelezi, ili waweze kwenda
na kasi ya utendaji wa majukumu yao. Lazima watu watendewe haki.
Upendeleo na uonevu uondolewe na masilahi kwa watumishi wa mahakama
yaboreshwe,” alisisitiza Jaji Sumari.
Aidha, aliiomba serikali pindi inapoanzisha wilaya na mikoa mipya
nchini, lazima izingatie uwepo wa majengo ya mahakama katika maeneo
husika, ikiwa ni pamoja na kuweka vifaa vya teknolojia ya kisasa, ili
kurahisisha utendaji kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo, alihimiza mahakama
za Mwanza kutafutiwa majengo sehemu nzuri na bora ili mhimili huo uweze
kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi bila kuingiliwa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment