Home » » MBOWE ANUSURIKA KIFO AJALINI

MBOWE ANUSURIKA KIFO AJALINI

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka jijini Mwanza kwenda wilayani Ngara, Kagera kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 6 mchana, umbali wa kilometa mbili kutoka Kata ya Katoro, Geita na inadaiwa kuwa gari alilokuwa akitumia limeharibika sehemu ya mbele.
Taarifa za uhakika kutoka eneo la tukio zimeeleza kwamba chanzo cha ajali hiyo iliyosababishwa na mwendesha pikipiki yenye namba za usajili T 212 BFR aliyefahamika kwa jina la Sayi Kahindi (32) mkulima, mwenyeji wa Kijiji cha Inyala kuingia ghafla barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati ajali hiyo ikitokea alikuwa akielekea wilayani Ngara kwa ajili ya mikutano ya
Operesheni M4C Pamoja Daima iliyoanza hivi karibuni nchi nzima.
Inadaiwa kwamba, Mbowe katika safari hiyo alikuwa akitumia gari la Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA) lenye namba za usajili T 217 CPB.
Baada ya ajali hiyo Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Kilimanjaro alipata gari jingine lenye namba za usajili T 888 CGT Pajero, mali ya mkazi wa Katoro, aliyejulikana kwa jina la Mbanju, ambalo lilimpeleka Ngara anakoendelea na mikutano ya kukijenga chama wakati dereva na gari lililopata ajali vikipelekwa kituo cha polisi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani Geita, John Mfinanga na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Kamanda Bwire, walithibitisha kuwepo kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali unaendelea.
“Nimezungumza na mwenyekiti mwenyewe Mbowe ameniambia ni kweli alipata ajali umbali wa kilometa mbili hivi kutoka mji wa Katoro akielekea Chato.
“Gari alilokuwa akisafiria limeharibika vibaya maeneo ya mbele. Pikipiki nayo imeharibika sana… wakati nawasiliana naye alikuwa ameshaondoka eneo la tukio akielekea Bihalamuro kwenda Ngara,” alisema Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje.
Kesho Mbowe anatarajiwa kutua Geita kwa helikopta ili kuhutubia mikutano ya hadhara katika mwendelezo wa shughuli za kukijenga chama chake
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa