MBUNGE wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), ametishia
kuwachukulia hatua kali makandarasi watakaojenga miradi ya zahanati na
wodi ya wazazi, inayotekelezwa na fedha za Mfuko wa Jimbo (CDCF), chini
ya kiwango.
Wenje, alitoa onyo hilo juzi alipozungumza na waandishi wa habari,
baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa miradi hiyo katika kata tatu
za Mahina, Isamilo na Buhongwa jijini hapa.
Alisema katika ziara yake hiyo aliyoongozana na wajumbe wa kamati ya
mfuko wa jimbo lake la Nyamagana wakiwemo wataalamu na watendaji wa
kata husika, alibaini mradi wa Mahina kuonekana kujengwa chini ya
kiwango.
“Mkataba wetu na makandarasi wa miradi yote hii ni kwamba, ikibainika
amejenga chini ya kiwango lazima abomoe na aanze kujenga upya kwa
gharama zake.
“Wodi ya wazazi Mahina tumeona kuna nyufa na mmomonyoko fulani wa
saruji. Sasa nimeagiza wataalamu wafanye ukaguzi, na ikibainika
mkandarasi amejenga chini ya kiwango lazima achukuliwe hatua kali.
Abomoe na kujenga kwa gharama zake,” alisisitiza Wenje.
Miradi hiyo na gharama zake kwenye mabano ni zahanati ya Isamilo (sh
mil. 15), wodi ya wazazi Mahina (sh mil. 20), zahanati ya Isebanda
Buhongwa (sh mil. 15).
Wenje alieleza kwamba fedha za mfuko wa jimbo lake zitatumika kujenga
miradi hiyo kuanzia msingi hadi kwenye linta, na baada ya hapo
Halmashauri ya Jiji la Mwanza itamalizia hatua iliyobaki.
“Mfuko wa Jimbo la Nyamagana tunapokea sh mil. 42 kwa mwaka, na fedha
hizi zote tunazielekeza kwenye miradi ya wananchi wetu. Malengo yetu
ni kupeleka maendeleo,” alisema.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment