Home » » PPRA YAKUSUDIA KUFUNGUA OFISI ZA KANDA

PPRA YAKUSUDIA KUFUNGUA OFISI ZA KANDA

Na John Maduhu, Mwanza
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), inakusudia kufungua ofisi za kanda kwa ajili ya kusogeza huduma hiyo na kuboresha utendaji wa kazi. Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanachama wa Chama cha Wakandarasi (CATA) Mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Ushauri wa PPRA, Dk. Lawrence Shirima, alisema ofisi hizo zinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Alisema ofisi hizo zitafunguliwa katika Mikoa ya Mwanza kwa ajili ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Iringa kwa ajili ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Arusha kwa ajili ya Kanda ya Kaskazini na zile za Dar es Salaam ambazo ziko kwa ajili ya kushughulikia Mikoa ya Pwani.

Alisema kufunguliwa kwa ofisi hizo, kutawasaidia wadau kupata huduma kwa haraka toka PPRA na kushughulikia kwa haraka matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika masuala ya ununuzi ikiwa ni pamoja na rufaa na kuchukua hatua kwa wahusika ambao wamekuwa wakikiuka sheria za ununuzi ya umma.

Kuhusu wakandarasi, aliwataka kujiamini na kuzingatia sheria kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakilazimika kutoa rushwa kwa ajili ya kupata zabuni wakati ni haki yao.

“Wakati mwingine wakandarasi wamekuwa wakiingia katika mtego wa kutoa rushwa kwa ajili ya kupata zabuni, mnapashwa kuelewa utaratibu mzima unaotumika kwa ajili ya kupata zabuni na msibabaishwe kwa ajili ya kujengewa mazingira ya kutoa rushwa,” alisema Dk. Shirima.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CATA, William Ngowi, alisema waliamua kuomba mafunzo toka PPRA pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kuwajengea uwezo na waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika majukumu yao ya kazi.

Alisema mafunzo yatakayotolewa na PPRA pamoja na TAKUKURU yatawasaidia wakandarasi katika kazi zao za kila siku na kuwataka wawe na umoja kwa ajili ya kupigania haki zao na taaluma yao.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa