Watu
wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa vibaya
katika ajali ya mabasi mawili yakugongana uso kwa uso katika kijiji cha
Kamanga, Sengerema mkoani Mwanza saa nne asubuhi jana.
Akizungumzia
ajali hiyo, shuhuda aliyekuwa katika pikipiki na kunusurika kugongwa na
mabasi hayo, Philipo Budeba, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo
kasi wa mabasi yote mawili.
“Mimi
nilikuwa naendesha pikipiki, mbele yangu kulikuwa na basi la Mkombozi
Trans lenye namba T540 DLF na nyuma kulikuwa na Basi la Walawi Express
lenye namba T167 CSN yote yalikuwa na mwendokasi," alisema Budeba.
"Dereva
wa Mkombozi ndiye aliyetaka kupita gari lingine, lakini ilishindikana
na kusababisha magari hayo kuvaana... mimi nilijirusha kwenye kilima cha
pembeni mwa barabara."
Naye
abiria wa Mkombozi Trans iliyokuwa ikitokea Kanyara Buchosa, Sengerema,
Fransisco Kansola alisema tabia ya madereva kushindwa kuchukua
tahadhari na kujali kuwahi abiria ndiyo chanzo cha ajali hiyo.
Walawi Express lilikuwa likitoka Mwanza kwenda Nemba wilayani Biharamulo.
Akithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
alisema dereva wa basi la Walawi, Frank Kimboka ni miongoni mwa majeruhi
wanane wa ajali hiyo baada ya kujeruhiwa miguu yote.
“Waliofariki
ni dereva wa basi la Mkombozi Trans aliyefahamika kwa jina la Simon
Mdalesalamu na mwanamke aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 20,"
alisema Kamanda Msangi.
Majeruhi
watatu wametajwa kuwa ni Frank Mushi aliyevunjika miguu yote miwili,
Isaack Hamisi (22) mkazi wa Nyasaka wilayani Ilemela na Mwinyi Ismail
(50) aliyevunjika miguu yote miwili, alisema Kamanda Msangi.
"Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi hayo.”
Aidha,
ajali hiyo ilitokea wakati mkoa wa Mwanza ukizindua maadhimisho ya wiki
ya Nenda kwa Usalama Barabarani, yenye kaulimbiu inayosema ‘Zuia ajali,
tii sheria, okoa maisha'.
Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu.
Kijukuu
0 comments:
Post a Comment