Tone

Tone
Home » » POLISI WANNE MBARONI KUFYATUA RISASI OVYO

POLISI WANNE MBARONI KUFYATUA RISASI OVYO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.  


ASKARI Polisi wanne wa Kituo Kikuu cha Polisi Nyamagana jijini Mwanza, wametiwa mbaroni kwa amri ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, kwa tuhuma za kufyatua risasi ovyo na kumjeruhi mke wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo Mapya Kata ya Mabatini.
Mwanamke huyo, Esther Ntobi, alijeruhiwa na askari hao walipofyatua ovyo risasi zaidi ya 10 sambamba na kuharibu mali za raia mtaani.
Askari hao ambao hata hivyo, majina yao hayakutajwa pia wanadaiwa kufanya kitendo hicho wakiwa wamelewa wakati wa doria.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti huyo, Boniphace Ntobi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5: 25 usiku, akiwa nyumbani akila chakula na familia yake.


Ntobi alisema alisikia kishindo akatoka nje na kukuta gari namba T 394 Toyota Hiace lililokuwa likiendeshwa na Iman Shabani Sinzya likiwa limegonga nyumba yake, ndipo alipoamua kupiga simu Kituo cha Polisi Mabatini na kutoa taarifa kwa mkuu wa kituo hicho.

“Alinijibu nisubiri kwa dakika 45, ili alishugulikie suala hili, na kweli alifika na kunitaka nisubiri askari wa usalama barabarani wafike… wakati tukisubiri yalifika magari mawili ya polisi na walishuka na kuanza kuuliza na ghafla walianzisha mzozo dhidi ya mjumbe wangu wa Serikali ya Mtaa, Kulwa Kisura na kuanza kumpiga, nilipowauliza nini tatizo na mimi wakanipiga huku wengine wakifyatua risasi hewani, zingine zikielekezwa ndani ya nyumba yangu,” alisema.

Ntobi alisema mkewe baada ya kuona anapigwa, aliuliza sababu za kupigwa, na yeye aliambulia kichapo na kuvuliwa nguo na alipokimbilia ndani walimfuta huku wakimrushia risasi na kumpiga mguu wa kushoto.

Diwani wa Kata ya Mabatini, Lucas Mbeye, alisema alisikia milio ya risasi iliyoanza saa sita usiku na kuibua taharuki kubwa kwa wakazi wa kata hiyo, kwa kudhani majambazi wamevamia maeneo hayo.

Mbeye aliiomba serikali kuwachukulia hatua kali askari hao kwa kukiuka maadili ya kazi yao. 

Katika eneo la tukio Nipashe ilishuhudia maganda 15 ya risasi yanayoaminika ni ya bunduki aina ya SMG na risasi moja ambayo haijatumika huku wakazi wa mtaa huo wakilaani kitendo hicho.

Esther amelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando kwa ajili ya matibabu.
Kamanda Msangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa askari hao hawakutumwa na Jeshi la Polisi kufanya tukio hilo, na kwamba ikithibitika wamefanya tukio hilo kwa makusudi, watachukuliwa hatua za kinidhamu.


Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa