George Binagi @BMGHabari
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika
MISA tawi la Tanzania (MISA Tanzania), umeonesha kwamba bado kuna
changamoto kwenye upatikanaji wa taarifa za umma katika ofisi mbalimbali
za serikali nchini.
Matokeo ya utafiti huo yanaashiria kwamba bado hakuna uwajibikaji wa
moja kwa moja kwenye sheria ya Haki ya kupata taarifa ya mwaka 2016 na
pia sera ya serikali kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kutoa
taarifa za umma.
Ripoti hiyo ya MISA Tanzania ya mwaka 2017 ililenga kubaini ni ofisi
gani ya serikali kati ya Serikali Kuu (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa) na
Serikali za Mitaa (Ofisi za Halmashauri za Majiji na Manispaa) inatoa
taarifa za umma kwa urahisi na ipi ni kikwazo kwa utoaji wa taarifa
hizo.
Utafiti huo uliodumu kwa muda wa siku 21 ulihusisha mikoa saba ambayo
ni Dodoma, Mbeya, Kigoma, Arusha, Mwanza, Mtwara pamoja na Dar es
salaam ambapo watafiti walitumia njia za simu, barua pepe na ana kwa ana
kuomba na kufuatilia taarifa katika ofisi husika.
Maksi za chini kwenye utafiti huo zilikuwa ni 0 na maksi za juu
zilikuwa ni 20 ambapo kuliwa na dodoso mbili za utafiti na hivyo kufanya
jumla ya maksi za juu kuwa 40. Ufafanuzi wa maksi hizo ni kwamba ofisi
iliyopata maksi 0-6 inaashiria ina usiri katika utoaji ya taarifa za
umma, maksi 07-13 ni ofisi iliyoonesha kiwango cha kawaida katika utoaji
wa taarifa za umma na maksi 13-20 ni ofisi iliyoonesha uwazi wa kutia
matumaini katika utoaji wa taarifa za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ilipata maksi 16/40 huku Halmashauri
ya Manispaa ya Dodoma ikipata maksi 25/40 na hivyo ofisi ya Manispaa ya
Dodoma kuongoza kwa utoaji wa taarifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ilipata maksi 21/40 huku ofisi ya
Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikipata maksi 36/40 hivyo ofisi inayotoa
taarifa za umma kwa uwazi mkoani Mbeya kuwa halmashauri ya Jiji la
Mbeya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ilipata maksi 31/40 na Ofisi ya
Manispaa ya Kigoma ikipata maksi 13/40 na hivyo kufanya ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma kuwa ofisi inayotoa taarifa za umma kwa uwazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilipata maksi 31/40 na Ofisi ya
Halmashauri ya Jiji la Arusha ikipata maksi 30/40 na hivyo kufanya Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwa ofisi inayotoa taarifa za umma kwa
uwazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ilipata maksi 09/40 na Ofisi ya
Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikipata maksi 09/40 na hivyo kuashiria
kwamba ofisi zote zina usiri kwenye utoaji wa taarifa za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ilipata maksi 12/40 na Ofisi ya
Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara kupata maksi 08/40 na kuashiria kwamba
ofisi zote zina usiri kwenye utoaji wa taarifa za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ilipata maksi 03/40 na Ofisi
ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaa ikapata maksi 22/40 na hivyo
kufanya ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuwa ofisi
inayongoza kutoa taarifa za umma.
Utafiti huu unaashiria kwamba asilimia kubwa ya wananchi hawanufaiki
moja kwa moja na sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 katika
ofisi za umma huenda kutokana na kutoijua vyema sheria hiyo jambo
linalosababisha taarifa zenye maslahi kwa umma kuendelea kuwa siri na
wakati mwingine kuibua mkanganyiko katika jamii.
Baadhi ya viongozi wa serikali nao bado wanaonekana kuwa wagumu
katika utoaji wa taarifa za umma huenda kutokana na kutoitambua vyema
sheria hiyo hivyo kuna kila sababu pande zote mbili kwa maana ya
viongozi na wananchi kuendelea kujengewa uwezo ili kuitambua vyema kwa
ajili ya manufaa ya jamii, kwani utoaji wa taarifa kwa uwazi ni
kichocheo cha maendeleo.
Taasisi ya MISA Tanzania inahimiza ripoti ya utafiti huo uliotokana
na mkoa mmoja mmoja kila kanda nchini, kutumiwa na ofisi nyingine katika
kujitathmini namna zinavyotoa taarifa zake kwa umma huku ikitaka
teknolojia kupewa kipaumbele ikiwemo matumizi ya barua pepe badala ya
wananchi kujazana kwenye ofisi za serikali kufuatilia majibu kutoka kwa
watumishi wa serikali na hivyo kupoteza raslimali pesa na muda.
PICHA: Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Salome Kitomari
0 comments:
Post a Comment