Na Benny Mwaipaja, WFM, Mwanza
Wizara
ya Fedha na Mipango yawataka wastaafu wanalipwa na Hazina ambao
hawajahakikiwa katika mikoa ambayo zoezi hilo limeshafanyika na
wanauwezo wa kufika katika maeneo ambayo zoezi hilo linaendelea ,
wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuhakikiwa.
Wito
huo umetolewa mkoani Mwanza na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali,
Msaidizi, Bw. Stanislaus Mpembe wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uhakiki
wa Wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango katika Kanda ya
Ziwa, mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita.
Mpembe
alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa wastaafu na Serikali kwa ujumla
kwani limelenga kuiwezesha Wizara ya Fedha na Mipango kuhuisha taarifa
za Wastaafu, kupata orodha sahihi ya wastaafu wanaolipwa na Wizara hiyo ili Serikali iweze kuwalipa wale wote wanaostahili.
Alifafanua
kuwa suala la uhakiki ni la lazima na kuwaomba wastaafu wajitokeze kwa
wingi kwani baada ya zoezi hilo kumalizika nchi nzima wastaafu ambao
hawatahakikiwa watafutwa katika mfumo wa malipo.
“Naomba
wastaafu wote wajitokeze katika Halmashauri zilizotangazwa, hata
wasiokuwa na nyaraka wajitokeze wataelekezwa mahali wanapoweza kupata
nyaraka zote muhimu” aliongeza Bw. Mpembe.
Alisema
kuwa wagonjwa na wasiojiweza wametengewa siku ya Ijumaa ambayo ni siku
ya mwisho ya uhakiki, ambapo watakuja ndugu au jamaa zao watakaotoa
taarifa sehemu walipo hususani waliopo hospitalini na sehemu ambazo
zinaweza kufikika kwa karibu na wahakiki ili nao wahakikiwe.
Naye
Mstaafu John Msanja, pamoja na kuomba serikali iwafikirie kuwaongezea
pensheni ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayowakabili,
aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na
waratibu kwa kuendesha zoezi hilo kistaarabu pamoja na kutoa kipaumbele kwa wagonjwa na wasiojiweza ambao waliweza kufika katika eneo hilo kwa lengo la kuhakikiwa.
Alisema
kuwa zoezi hilo linaonesha ni namna gani Serikali inawajali wazee
waliolitumikia Taifa kwa muda mrefu kwa kuhakikisha ni namna gani
wanapata stahili zao kwa wakati.
Zoezi
hili lilianza Oktoba, 2016 katika Mkoa wa Pwani na kuendelea katika
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini.
Mpaka sasa wastaafu wa mikoa 13 ya Tanzania Bara wameshahakikiwa.
Baada ya uhakiki kumalizika Kanda ya Ziwa, zoezi hili litaendelea katika mikoa ya Kigoma na Tabora.
0 comments:
Post a Comment