Na Benedict Liwenga-MAELEZO
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Mhandisi
Stella Manyanya leo amewasili Mkoani Kagera na kutembelea miundombinu ya sekta
ya elimu ili kujionea namna serikali inavyorejesha hali kama awali kutokana na
tetemeko la ardhi lililotokea September 10 mwaka huu.
Akiwa katika shule ya sekondari ya Ihungo, Mhandisi Manyanya
amewataka wakandarasi waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi upya wa majengo
mapya ya Shule za Ihungo na Nyakato kujenga kwa kuzingatia viwango sahihi
kulingana na maelekezo ya wataalam wa miamba.
“Mmepewa dhamana ya kusimamia ujenzi upya wa shule hii,
nawaombeni muzingatie viwango sahihi wakati mnajenga hasa kwa kuangalia
mapendekezo ya wataalam wa miamba waliyoyatoa ili kuyaweka majengo katika hali
ya usalama” Alisema Mhandishi Manyanya.
Aidha Mhandisi Manyanya amewatahadharisha wakandarasi wenye
tabia ya kudokoa vifaa vya ujenzi kutothubutu kufanya hivyo kwani yeyote
atayeiba vifaa hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Katika kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu tofauti wanapata
elimu sawa Mhandisi Manyanya amewataka walimu wa shule ya msingi Mgeza Mseto
kutenda haki sawa wanafunzi wote bila kujali aina ya ulemavu alionao
mwanafunzi.
Katika hatua nyingine Mhandisi Manyanya amezitaka shule hasa
za sekondari nchini kuanzisha mashamba darasa yatakayowawezesha wanafunzi
kujifunza kwa vitendo shughuli za kilimo na kusaidia kuifanya shule kuwa na
hifadhi ya kutosha ya chakula.
Kwa upande wa walimu Mhandisi Manyanya amewapongeza walimu
wa wilaya ya Bukoba kwa kujituma na kuwekeza katika kilimo cha migomba na
kuwataka walimu kote nchini kuiga mfano huo ili kuwa na chakula cha kutosha na
kujiongezea kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.
0 comments:
Post a Comment