Na JUDITH NYANGE-MWANZA
WATU 13 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la Super Shem
lenye namba za usajili T 874 CWE lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea
Mwanza na Hiace yenye namba T 368 CWQ iliyokuwa ikitoka Jijini Mwanza
kuelekea Wilaya ya Kwimba.
Katika ajali hiyo mfanyabaishara ndogo ndogo maarufu machinga, Peter
Tobari, aliokoa maisha ya abiria zaidi ya 30 kwa kumsaidia dereva wa
basi la Super Shem ambaye alikuwa amekandamizwa miguu na basi hilo baada
ya kugongana na Hiace.
Ajali hiyo imetokea siku mbili baada ya ile ya basi la Kampuni ya New
force iliyotokea mkoani Njombe ikihusisha basi lenye namba T 429 DEU
lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma, ambapo
watu 12 walifariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa vibaya.
Katika ajali ya Mwanza, gari dogo aina ya Hiace liligongana uso kwa
uso na basi la Super Shem na kusababisha vifo hivyo na wengine 10
kujeruhi.
Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kidogo cha mabasi
cha Hungumalwa njia panda ya Shelui na Mwamashimba katika Kijiji cha
Mwamaya wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Ilielezwa katika tukio hilo, dereva wa Hiace aliingia barabara kuu ya
Mwanza-Shinyanga bila kuchukua hadhari na hivyo kukutana na basi hilo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya ajali hiyo watu 10 walikufa papo
hapo na wengine 11 kujeruhiwa, ambapo mmoja alifariki dunia akiwa njiani
akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wawili walifariki dunia
wakati wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa matibabu zaidi.
SIMULIZI
Akisimulia ajali hiyo, mfanyabiashara Tobari alisema baada ya magari
hayo kugongana dereva wa basi lao alijaribu kuliepusha kupinduka, lakini
alishindwa kutokana na kubanwa miguu.
Macginga huyo alishika usukani na kuliongoza gari hilo hadi
kuliegesha pembeni na kufanikiwa kunusuru maisha ya abiria waliokuwemo
ndani ya basi hilo.
“Baada ya kugongana, upande wa dereva wa gari la basi letu (Super
Shem) uliharibika vibaya na wakati dereva akijaribu kusogeza gari
hilo pembezoni mwa barabara ili lisipinduke alishindwa kutokana na bodi
la mbele na usukani wa gari kumkandamiza miguu.
“Nilipoona usukani umeshuka na dereva hawezi kufanya lolote
niliushika na kumsaidia kulisogeza pembeni mpaka nilipofanikiwa kuegesha
na kulinusuru lisipinduke na kuhatarisha zaidi maisha ya abiria
wenzangu.
“Baada ya hapo nilimtoa dereva ambaye alikuwa amekandamizwa sana
sehemu ya miguu na kutafuta usafiri kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya
Wilaya ya Misungwi ambako anatibiwa,” alisema.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Dk. Bethod
Nchemba, akizungumzia ajali hiyo alisema walipokea majeruhi 10
wakiwemo wanaume na wanawake watano ambapo mmmoja alikuwa na hali mbaya
na alifariki akiwa mapokezi wakati akiendelea kupewa huduma.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Monica Shija, Christina
Costantine, Theresia Majenga wote wakiwa wakazi wa Kijiji cha Gulumwa
wilayani Kwimba, Lwinzi Kope mkazi wa Kijiji cha Chaselwe, Mabula Magi
wa Rukwa, Isaya Deogratius mkazi wa Mbande, Moses Kamel wa Kijiji cha
Bupamwadomu, George Ndila mkazi wa Sangu, Kondakta wa hiace
aliyefahamika kwa jina moja la Poni pamoja na mtu mmoja mwanaume, mama
mmoja na mtoto ambao hawajafahamika wote wakiwa ni abira wa Hiace.
Alisema majeruhi watatu wanaendelea vizuri na matibabu katika
hospitali hiyo na miili tisa kati ya 11 imeshatambuliwa isipokuwa mwili
wa mama mmoja na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 5 na majeruhi
sita wamelazimika kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa
matibabu zaidi.
MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment