Mfahamu binti Johari Swedy, mwanafunzi na mkazi wa Jiji la Mwanza. Ni binti anaestahili kuigwa na wengine kutokana na juhudi na malengo yake maishani.
Na George Binagi -GB Pazzo
Johari Swedy (kushoto) akizungumza na GB @BMG (kulia) alipokuwa katika eneo la Ahsante Moto Jijini Mwanza.
Kutana na
binti Johari Swedy (19), mkazi wa Jiji la Mwanza. Alizaliwa mwaka 1997. Ni mwanafunzi
ambae historia ya masomo yake ilianzia shule ya msingi Mabatini aliposoma
darasa la kwanza hadi darasa la saba na baadae akajiunga na shule ya sekondari
Mtoni zote za Jijini Mwanza ambapo alisoma kidato cha kwanza hadi kidato cha na
nne.
Baadae
alijiunga na masomo ya kidato cha tano katika shule ya sekondari Lugeye kabla
ya kuhamia Mwanza Sekondari zote pia za Jijini Mwanza, mwaka huu kwa ajili ya
kuhitimisha masomo yake ya kidato cha Sita.
Sifa kubwa
aliyonayo binti huyu ni kuwa miongoni mwa mabinti wanaopenda kusoma masomo ya
sayansi hapa nchini. Alijiunga na masomo yake ya kidato cha tano baada ya
kufaulu vizuri masomo ya sayansi ambayo ni Fizikia, Kemia na Baiolojia kwa
maana ya mchepuo wa PCB.
Kama ilivyo
kwa wanafunzi wenye malengo ya kufanikiwa maishani, binti huyu anazo ndoto
zake. Mosi ni kujikiza katika kipaji chake cha utangazaji baada ya kuhitimu
masomo yake ya elimu ya juu. Kipaji ambacho ni utangazaji. Lakini pia anasema
pamoja na ndoto hiyo, anayo malengo mengine ya kuwa daktari ama mfamasia.
“Mimi ndoto
zangu ni kuwa mtangazaji. Vile vile nina malengo zaidi kama si kuwa mtangazaji
labda niwe mfamasia au niwe daktari”. Anasema binti huyu na kutanabaisha kwamba
kipaji chake cha utangazaji kilianza kuonekana baada ya kujiunga na Mtandao wa Vijana
na Wanahabari Watoto mkoani Mwanza (Mwanza Youth and Chilren Network-MYCN)
ambapo alikuwa akiongoza kipindi cha watoto (Sayari ya Watoto) cha redio na
luninga kupitia Metro Fm na Barmedas Tv zote za Jijini Mwanza.
Binti huyu
anaenda mbali zaidi na kuwahamasisha wanafunzi wa kike nchini, kupenda kusoma
masomo ya sayansi kutokana na umuhimu wake na anawatoa hofu wale wenye mtizamo
hasi juu ya masomo ya sayansi kwamba masomo hayo ni magumu.
“Masomo ya
sayansi kiukweli watu wanayachukulia kuwa ni masomo magumu, lakini ukiamua
unaweza, napenda wasome masomo ya sayansi kwa sababu ni masomo mazuri sana na
kama ni mtu kweli unapenda kusoma na unapenda ndoto zako zitimie, soma masomo
ya sayansi maana yanakuruhusu kufanya kazi yoyote ile”. Anasema binti huyu.
Mbali na
masomo, binti huyu anao mwamko mkubwa wa kujifunza mambo mbalimbali kuhusu
maisha. Akiwa likizo anapenda sana kujifunza kuhusu kazi za nyumbani pamoja na
ujasiriamali. Anasema muda wake wa likizo huutumia katika kusoma masomo ya
ziada (tuition) na kumsaidia mama yake shughuli za gengeni (Mama lishe) katika
Mtaa maarufu wa akina mama na baba lishe wa Ahsante Moto uliopo stendi ya
zamani ya Tanganyika Jijini Mwanza.
“Mimi ni
mjasiriamali kutokana na kuwa namsaidia mama yangu shughuli mbalimbali za
kupika, nikiwa likizo. Kama sijaenda tuition (masomo ya ziada) nakuja kumsaidia
mama shughuli za upishi, najifunza pia mambo mengine kuhusiana na biashara,
anapokuwa hayupo mimi huwa naisimamia biashara kama ni ya kwangu”. Anaeleza binti
Johari.
Mama mzazi
wa Johari, aitwae Devota Alex maarufu kwa jina la Mama Taus ambae ni Mama lishe
katika eneo la Ahsante Moto Jijini Mwanza, anasema anajivunia juhudi za binti
yake katika kujifunza mambo mbalimbali muhimu katika maisha ambayo anasema yanamjengea
binti huyu msingi imara kwa ajili ya maisha yake ya baadae.
0 comments:
Post a Comment