POLISI mkoani Mwanza imemuua jambazi baada ya mtu huyo akiwa na
wenzake wawili kurushiana risasi na polisi waliokuwa doria baada ya
kushindwa kutii amri ya kusimama walipotakiwa kufanya hivyo na polisi.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza,
Ahmed Msangi alisema mauaji hayo yalitokea Mei 31, mwaka huu saa 4.10
usiku katika Mtaa wa Ilemela katikati ya barabara inayopita kati ya eneo
zilipo ofisini za Radio Free Afrika (RFA) na Kiwanda cha Samaki cha
Mwanza.
Alisema polisi waliokuwa doria katika eneo hilo waliwatilia mashaka
watu watatu waliokutana nao usiku huo wakiwa wamebeba sanduku na
walipoamriwa kusimama, hawakutii. “Hawakutii, badala yake watu wale
waliongeza mwendo, huku mmoja wao akitoa mfuko uliokuwa na kitu, kumbe
ilikuwa ni bunduki na kuanza kurushiana risasi na polisi,” alieleza
Kamanda Msangi.
Alisema mtu huyo alifyatua risasi kati ya tatu hadi nne kwa polisi,
lakini hazikuleta madhara kwa walinzi hao wa usalama wa raia waliomuua
kujibu mapigo kwa kumpiga risasi na kumuua papo hapo huku wenzake wawili
wakikimbia na kuelekea kusikojulikana.
Alisema baada ya tukio hilo, polisi walimkuta jambazi huyo akiwa na
silaha aina ya SMG iliyochakaa na namba zake zikiwa zimefutika ikiwa na
magazini yenye risasi 16. Alisema upelelezi kwa ajili ya tukio hilo
unaendelea.
Kamanda Msangi alisema silaha iliyokamatwa hutumika kwenye majeshi na
kuwa mwananchi wa kawaida haruhusiwi kutumia silaha ya aina hiyo.
“Tutapeleka silaha hii kwa wataalamu kwa ajili ya kuitambua maana
bunduki ya aina hii hatuna kwenye majeshi yetu,” alisema kuongeza kuwa
mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa
ajili ya utambuzi.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment