Na Fredrick Katulanda, Mwanza
ALIYEKUWA Mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Anthony Mbassa alifariki dunia
jana usiku akiwa usingizini nyumbani kwake.
Taarifa zilizopatikana kutoka Biharamulo na kuthibitishwa na Msemaji
wa familia, Pendo Ngonyani, zilieleza kuwa kifo cha Dk. Mbassa
kilifahamika alfajiri ya jana.
Alisema watoto walipokwenda kumuamsha hakuamka hali iliyowalazimu
kuwamuita mama yao ambaye aliwasiliana na madaktari wa Hospitali ya
Biharamulo na kuthibitishwa kuwa alikuwa amefariki dunia.
Dk. Mbasa ambaye alikuwa mbunge mwaka 2010 baada ya kushinda
uchaguzi mkuu, hakurejea kwenye ubunge baada ya kuangushwa na mshindani
wake, Oscar Mkasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba, 2015.
Akizungumzia kifo hicho, Pendo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la
Wanawake wa Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kagera, alisema Dk. Mbassa
alifariki dunia akiwa usingizini.
Pendo alisema haijafahamika sababu ya kifo chake ingawa familia
imedokeza inataka uchunguzi ufanyike kubaini sababu ya kifo hicho.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, juzi mkewe akiwa kazini, yeye
(Dk. Mbasa) alitoka na kurudi jioni saa 12 na kuacha gari lake
nyumbani na kwenda ambako hakujajulikana. Alirudi nyumbani saa 5.00
usiku akiwa akionekana kuwa amelewa.
“Nimeelezwa kuwa baada ya kuacha gari alitoka kwa mguu kuanzia hiyo
saa 12 na kurejea yumbani saa 5.00 usiku. Haijajulikana alikwenda
wapi lakini alirejea akiwa amekunywa alikuwa akihangaika na ilidhaniwa
ni hali ya pombe, ndiyo hivyo asubuhi alikutwa akiwa amefariki dunia.
“Leo alikuwa na safari ya kwenda Bukoba kuwasiliana na mawakili
wake kwa ajili ya kushughulikia madai ya fidia ya Sh milioni 60 za
gharama za kesi namba 5/2010, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge
wa CCM jimbo hilo, Oscar Mkasa,” alisema.
Alisema kinachosubiriwa hivi sasa ni ndugu na jamaa kupanga utaratibu wa maziko.
CHANZO GAZETI LA MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment