MKOA wa Mwanza leo utaendesha kampeni maalumu ya kugawa dawa za
kukinga na kutibu magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo kwa watoto
wenye umri wa miaka mitano hadi 14.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mratibu wa magonjwa ambayo hayapewi
kipaumbele, Dk Donald Leonard, alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari juu ya maandalizi yaliyofanywa na mkoa kwenye kampeni ya ugawaji
dawa kwa watoto hao.
Alisema kazi hiyo ya kugawa dawa hizo ambayo litafanyika kwenye shule
zote za msingi itaanza saa moja asubuhi kwa maandalizi ya kuwapa
chakula wanafunzi kisha kuwapa dawa kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 11
jioni.
“ Nitoe ombi kwa wazazi wahakikishe kuwa wanawaandalia watoto chakula
kabla hawajapatiwa dawa ya kukinga maambukizi ya kichocho na minyoo ya
tumbo”, alisema Leonard.
Alisema ni muhimu kwa watoto kupata dawa hizo kwa sababu wasipozipata
kwa wakati minyoo ya tumbo inaweza kusababisha utumbo kuziba na utumbo
wa mtu unaweza kukatwa.
“Minyoo ikiingia kwenye ubongo huleta dalili kama za kifafa, minyoro
pia huathiri ini na endapo muathirika akichelewa kupata matibabu anaweza
kufa”, alisisitiza Leonard.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Clodwig Mtweve, amewataka wazazi
kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata dawa za kutokomeza magonjwa ya
kichocho na minyoo ya tumbo kwa ajili ya kulinda afya zao.
Alisema utafiti zilizofanywa mwaka 2005 zinaonesha kuwa maambukizi ya
kichocho nchini yapo kati ya asilimia 12.7 hadi 87.6 na kuwa ugonjwa
huo umeenea zaidi maeneo ya kando ya Ziwa Victoria.
“Kwa mujibu wa utafiti huo, kiwango cha maambukizo ni zaidi ya
asilimia 80 na kwa minyoo ya tumbo ni hadi asilimia 100 kwa baadhi ya
maeneo”, alisema Mtweve.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment