Home » » MIAKA 21 TANGU KUZAMA MELI YA MV.BUKOBA, JE USAFIRI WA MAJINI NCHINI NI SALAMA?

MIAKA 21 TANGU KUZAMA MELI YA MV.BUKOBA, JE USAFIRI WA MAJINI NCHINI NI SALAMA?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Miaka miwili iliyopita, katika kuadhimisha kumbukumbu ya kuzama Meli ya Mv.Bukoba, kwa msaada wa mtandao, niliandaa makala haya hivyo nimehariri kidogo ili kuendana na wakati, japo uhalisia wake uko pale pale.
Na George Binagi

Mei 21 Mwaka 1996 Taifa la Tanzania liligubikwa na Msiba Mkubwa ambapo kila mmoja kwa nanma yake aliguswa na Msiba huo ambao uliyagharimu Maisha ya Mamia ya Wapendwa Wetu, baada ya Meli ya MV.Bukoba Kuzama hatua chache kabla ya kutua Nanga Mkoani Mwanza ikitokea Mkoani Kagera.

Meli ya Mv.Bukoba iliyoundwa mwaka 1979 ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850 na abiria 430 ilizama katika Maji ya Ziwa Victoria Mkoani Mwanza yapata umbali wa kilomita zipatazo 30 kutoka ufukweni mwa maji na kusababisha zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha katika Meli hiyo ambayo tangu kuundwa kwake hadi kuzama kwake ilikuwa na umri wa miaka 17. Jambo la butwaa hapa ni Idadi ya vifo na idadi ya abiria waliookolewa ukilinganisha na Uwezo uwezo wa Meli hiyo wa kubeba abiria 430).

Pengine tumezoea kuita kwamba Mei 21 Watanzania tunaadhimisha kumbukumbu ya kuzama kwa Meli hiyo ambayo iliigeuza taswira ya Mji wa Mwanza, kwani kwa waliokuwa Mwanza Mwaka huo walipigwa na Butwaa baada ya Uwanja Mkongwe wa Nyamagana ambao mara nyingi hutumika kwa shughuli za Kimichezo, pale ulipogeuka na ghafla na kutapakaa Maiti za wapendwa wetu, ama hakika inauma sana.

Wakati leo tunakumbuka tukio hili ambalo limeacha simanzi mioyoni mwetu, hebu tujiulize kwa pamoja; Kama ilivyo imani ya watalaamu wa masuala ya usafiri kwamba Usafiri wa Majini ndio usafiri salama kuliko aina nyingine ya usafiri, Je Kwa Tanzania imani hiyo ina mantiki yoyote kwamba vyombo vyetu vya usafiri wa majini ni salama?.

Lakini wakati tunatafakari suala hilo, pia tukumbuke kujiuliza sisi wenyewe bila kusubiri kusukumwa na mtu hususani wale wenye mamlaka ya kuleta matokeo chanya katika kuboresha hali ya usafiri majini Ikiwemo Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA  kwamba tulijifunza jambo lolote kutokana na ajali hiyo ya Mv.Bukoba?

Na Kama kuna jambo tulijifunza, je tumefanikiwa kulifanyia kazi ipasavyo jambo hilo? Je kuna hali yoyote ya uwajibikaji (kwa waliopewa dhana ya kusimamia sheria) katika kuzingatia sheria za usafiri na usafirishaji wa majini na nchi kavu? Je, tumekwisha jijengea hali ya kuchukua hatua za uokoaji pale tunapopatwa na majanga ya majini au nchi kavu?.

Lakini pia wapo waliohoji na bado wanaendelea kuhoji juu ya taarifa ama ripoti ya uchunguzi wa ajari hiyo ya Mv.Bukoba kama ulifanyiwa kazi ipasavyo? Lakini pia wakiwa bado wanaendelea kujiuliza ni ajari ngapi za vyombo vya majini zimetokea tangu kuzama kwa meli hiyo? Hapo nadhani nawe unazikumbuka ajali kadhaa ambazo tayari zimekwisha kutokea na kuyagharimu maisha ya Watanzania ikiwemo ile ya mv Spice Ireland iliyotokea Septemba 10 mwaka 2011 katika Mkondo wa Nungwi kaskazini Unguja Zanzibar.

Lakini yote Tisa, Kumi ni stofahamu iliyoibuka juu ya Chanzo cha ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea hapa nchini.Wapo waliosema ilikuwa ni Uzembe wa Wakaguzi wa na Waangalizi kwa maana ya Mamlaka husika, Wapo waliosema ilikuwa ni Uzembe wa Nahodha na Timu yake na wapo waliosema Chombo kilikuwa kibovu.

Wapo waliodai chombo hicho kilikuwa kimebeba Mizigo na abiria kuzidi uwezo wake na wapo waliodai kuwa abiria wenyewe walisababisha ajali hiyo kwani walilazimisha kupanda Melini ilihali chombo kilikuwa kimejaa huku mlolongo huo ukihitimishwa na wale waliohusisha ajali hiyo na Imani za Kishirikina.

Mimi nasema sina nia ya kuandika hayo yote kwa lengo la kumtafuta mchawi ila lengo langu ni kuyaweka wazi hayo yote ili kila mmoja kwa namna anavyohusika na anavyoweza kusaidia namna ya kufanya ili kuepukana na ajali kama hiyo ama kama ambavyo wengine husema tusiangalie tulipoanguka bali tuangalie tulipojikwaa.

Wapo wengi waliowapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao na mmoja wao ambae alimpoteza mpendwa wake katika maisha yake ni Mwanamitindo maarufu hapa nchini ambae pia anafanya shughuli zake barani Ulaya Flavian Matata ambae yeye alimpoteza Mama yake mzazi pamoja na binamu yake.

Pamoja na watu wengine, Matata amekuwa na desturi ya kukumbuka tukio hilo kwa kufika Mkoani Mwanza katika eneo la Igoma walikohifadhiwa watu waliopeza maisha katika ajali hiyo ya Mv.Bukoba ambapo pia maadhimisho ya kuwakumbuka hufanyiia kila mwaka, huku akibainisha kuwa ilimchukua miaka mingi hadi kuamini kuwa ni kweli hayuko na mama yake mzazi, kwa kusema kuwa ni miaka michache iliyopita ndiyo ameweza kuamini kama ni kweli hayuko na mama yake tena.Hakina inauma sana.


Yapo mengi ya kuzungumza na kuandika lakini swali la kujiuliza ni moja tu, miaka 21 mwaka huu 2016 tangu kuzama meli ya Mv.Bukoba Mei 21 mwaka 1996, Je usafiri wa majini ni salama hapa nchini ama tunasafiri kwa kudra za Mwenyezi Mungu? Mimi nihitimishe kwa kusema ni jukumu la kila mmoja wetu kwa kushirikiana na Mamlaka husika ikiwemo SUMATRA kuhakikisha kuwa usafiri wa Majini Unakuwa usafiri salama hapa nchini.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa