Mahakama
ya Tanzania inakusudia kuongeza idadi ya Majaji katika kanda yake ya
Mwanza ili kuongeza msukumo wa kumaliza kesi za mauaji kutokana na kanda
hiyo kuongoza kwa kuwa na kesi nyingi za mauaji nchi nzima.
Akizungumza
wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za kimahakama katika kanda ya
Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amesema
ataongeza idadi ya majaji katika kanda hiyo ili kesi hizo za mauaji
zimalizike kwa wakati.
Jaji
Mkuu pia ameiagiza Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kuzipa msukumo maalum
kesi za mauaji ili kuhakikisha zinamalizika mapema na kupunguza
mlundikano wa kesi katika mahakama za Tanzania.
Awali
akisoma taaarifa ya hali halisi ya kesi katika Mahakama Kuu kanda ya
Mwanza, Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo Mheshimiwa Robert Makaramba alisema
kanda ya Mwanza ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kesi nyingi za mauaji
nchini ambapo hadi kufikia Aprili mwaka huu kuna jumla ya kesi 512 za
mauaji.
Pamoja
na mkakati wa Jaji Mkuu kuongeza idadi ya Majaji ili kumaliza kesi
hizo, Jaji Mfawidhi wa kanda ya Mwanza alisema wameshachambua kesi hizo
za mauaji ambapo Jaji Kiongozi pia aliahidi kuwaongezea jumla ya Majaji
11 ili waweze kusaidia kusukuma kesi hizo.
Jaji
Makaramba alisema kati ya mwezi Juni na Julai jumla ya vikao 11
vinatarajiwa kukaa ili kusikiliza kesi 123 zilizopangwa kusikilizwa.
Alisema kati ya kesi hizo, 35 ni zile zitakazosikilizwa kwa mara ya
kwanza na kesi 88 ni zile zitakazosikilizwa mpaka mwisho.
Alisema endapo vikao hivyo vitafanyika kama ilivyokusudiwa vitasaidia kupunguza kesi zilizopo mahakamani kwa miaka mingi.
Hadi
kufikia mwezi April mwaka huu, Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ina jumla
ya kesi 2771 za aina zote zikiwemo zile za Madai ya kawaida, Madai ya
Ardhi na za jinai. Ili kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kesi hizo, kila
Jaji amepangiwa kusikiliza kesi 346. Kanda hiyo ina Majaji nane (8).
Jaji
Mkuu wa Tanzania ameanza ziara katika kanda ya Mwanza inayohusisha
mikoa ya Geita, Mwanza na Mara ambapo atakagua shughuli mbalimbali za
kimahakama katika kanda hiyo.
0 comments:
Post a Comment