Home » » UZEMBE KAMA HUU MV VICTORIA USIRUDIWE

UZEMBE KAMA HUU MV VICTORIA USIRUDIWE

MV Victoria 

Jana katika gazeti hili tulichapisha habari iliyokuwa ikielezea watumiaji wanaotegemea meli ya Mv Victoria, Jumatano walipata adha ya usafiri baada ya kusitishwa kwa safari ya kuelekea Mwanza, hatua iliyochukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwamba ilitoroshwa bila kukaguliwa.
Habari hiyo ilimkariri Ofisa Mfawidhi wa mamlaka hiyo mkoani Kagera, Kapteni Alex Katama akisema awali, meli hiyo ilizuiliwa Mwanza kwa ajili ya matengenezo na kwamba haikufanyiwa ukaguzi kabla ya kuruhusiwa na akisisitiza kuwa meli hiyo bado mbovu.
Ilielezwa kuwa ilipofika Bukoba ikitumia injini moja bila ruhusa ya mamlaka, waliizuia mpaka itakapofanyiwa ukaguzi na kujiridhisha.
Hadi inazuiliwa, ilikuwa ikijiandaa kwa safari hiyo ya Mwanza na tayari mizigo ilikuwa imeshapakiwa.
Hata hivyo, Meneja Masoko wa Shirika la Huduma za Meli, Obed Tirugumila alikaririwa akisema kuwa Mv Victoria ilifanyiwa matengenezo Mwanza, lakini haikufanyiwa majaribio na maofisa wa ukaguzi wa Sumatra akidai kuwa walisema hawana nafasi.
Hivyo, waliamua kufanya majaribio kwa kwenda Bukoba wakiwa na abiria na kufika salama.
Ni miaka 18 sasa tangu Meli ya Mv Bukoba izame ndani ya Ziwa Victoria Mei 21, 1996 ikitokea Bandari ya Bukoba kwenda Bandari ya Mwanza na kuua zaidi ya watu 1,000 kutokana na kuzidisha mizigo na abiria.
MV Bukoba ilizama ikiwa imebakisha umbali mfupi kufika Bandari ya Mwanza, lakini ukosefu wa vifaa vya uokoaji vilisababisha kuongezeka idadi ya watu waliokufa.
Waokoaji wa ajali hiyo walisubiriwa kufika nchini kutokea Afrika Kusini, ambao waliweza kuogelea na kuokoa baadhi ya maiti chache zilizokuwa zimezama umbali wa mita 25 chini ya maji.
Serikali ilimshtaki aliyekuwa nahodha wa Mv Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru, (sasa marehemu), Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari Gilbert Mokiwa; aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
Kama hiyo haitoshi, mwaka 2011 ajali nyingine mbaya ya Meli ya Spice Islander iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Pemba ilizama na kuua watu 240.
Tume iliyochunguza ajali ya meli hiyo ilisema meli hiyo ilibeba zaidi ya abiria 2,000 ingawa maelezo ya nahodha wa meli alidai kuwa melini kulikuwa na watu 500.
Mwaka 2012 Meli ya MV Skagit ilizama na kuua zaidi ya watu 30 japokuwa sababu za kuzama kwa meli hiyo inaelezwa kuwa ni hali mbaya ya hewa katika bahari siku ya tukio.
Matukio haya ya ajali yanatoa picha kwamba ajali nyingi zinazotokea nchini zinasababishwa na uzembe.
Tunasema uzembe kwa sababu tukio la Meli ya Mv Victoria kuruhusiwa kubeba abiria wakati ikiwa mbovu, linaonyesha wazi kuwa maofisa wanaohusika na meli hiyo walikuwa tayari kuua kwa sababu tu ama kutaka kupata fedha au sababu nyingine wanazozijua.
Pamoja na kuwa viongozi wa Serikali inapotokea ajali wamekuwa wepesi kutoa maneno ya matumaini kuwa watachukua hatua za kudhibiti ajali kama hizo zisitokee, lakini ukweli ni kwamba huwa maneno hayo yanaishia hapo hapo.
Tunashuhudia kila mara ajali nyingi zinaendelea kutokea kama vile hakuna hatua madhubuti zinazotakiwa kuchukuliwa, huku Serikali ikiunda tume ya kuchunguza ajali zinazotokea.
Mfano wa kushindwa kuchukuliwa hatua kuzuia ajali za majini ni pamoja na uamuzi wa Meli ya Mv Victoria kuruhusiwa kusafirisha abiria wakati ikiwa mbovu.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa