Tone

Tone
Home » » MWAKYEMBE AWAJIA JUU WAKANDARASI WAWILI

MWAKYEMBE AWAJIA JUU WAKANDARASI WAWILI

SERIKALI imewataka wakandarasi wenye zabuni ya ujenzi wa bandari mbili tofauti katika Visiwa vya Ntama na Lushamba, wilayani Sengerema mkoani Mwanza kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa.
Mwito huo ulitolewa juzi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kwa nyakati tofauti wakati akikagua hatua za ujenzi wa vivuko hivyo ambavyo vipo kwenye hatua za awali za ujenzi wake.
Vivuko hivyo vinajengwa na wakandarasi wawili wa Kampuni za Gemenen Engineering na Nangwm Engineering. Alisema kivuko cha Ntama kinatarajiwa kutumia kiasi cha Sh bilioni 2 wakati na kile cha Lushamba, kitatumia takribani Sh bilioni 1.2 na kwamba vinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba 2015.
Aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo ya ujenzi wa bandari kwa muda uliopangwa, na kwamba serikali haitaki kusikia visingizio vya aina yoyote ili wananchi wasiendelee kupata shida.
Awali akizungumza Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema wananchi wa eneo hilo, wamekuwa wakipata shida kwa muda mrefu ya usafiri, kutokana na kutokuwa na sehemu mahususi ya kusubiria meli.
“Wananchi wa eneo hili wameteseka sana na usafiri, wanashindwa kusafirisha mazao yao kwenda Mwanza kutokana na miundombinu kuwa mibovu na umbali mrefu wa kutumia barabara,” alisema Dk Tizeba.
Aliongeza kuwa mvua zinaponyesha watu hukosa sehemu ya kujikinga kutokana na mazingira ya sehemu yenyewe hivyo kuwa na wakati mgumu na unaosababisha kero kwao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Bandari kuu ya Mwanza (TPA), Patrick Paul alisema gati ya Ntama itakuwa na urefu wa mita 64 kuingia ndani ya Ziwa na upana wa mita 6.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa