ASKOFU mkuu wa Jimbo la Mwanza, Juda Thadeus Ruwaich amewahimiza wanafunzi wa vyuo vikuu kujishughulisha na kujibidiisha kujua lugha zaidi ya moja ili kuendana na soko la ajira.
Aidha, amewataka kuhakikisha wanapambana na nchi zote za Afrika Mashariki na duniani kote, ambao hutumia lugha mbalimbali katika biashara, uchumi, taaluma na hata mwingiliano wa nchi mbalimbali.
Askofu Ruwaich, ameyasema hayo wakati wa sherehe za Kumbukumbu ya Mtakatifu Agustino wa Hippo, ambaye ndie mlezi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino kilichopo Mwanza hivi karibuni, tukio lililokwenda pamoja na kumtangaza Makamu mkuu mpya wa chuo hicho, Mchungaji Dk. Thadeus Mkamwa.
Askofu Ruwaich, alisema ili kuingia katika ushindani wa ajira, lugha kama Kifaransa, Kijerumani, Kiswahili na Kingereza ni muhimu kwa sasa, kwani Tanzania haishindani na nchi za Afrika Mashariki tu bali duniani kote.
“Kuna siku nilikuwa Kigali na nilishuhudia wanafunzi wengi wa vyuo vikuu kutoka nchi ya Tanzania wanashindwa hata kujieleza, kutokana na kutojua lugha ya Kiingereza vizuri,” alisema Askofu Ruwaich.
Naye Mtaalam wa saikolojia wa Chuo cha Mtakatifu Augustino, Lukas Maziku, amelaumu mfumo mbovu wa elimu na watu wanaoutengeneza mfumo huo.
Alisema ni lazima programu za vyuo vikuu ziendane na mfumo wa soko la ajira, lakini changamoto kubwa hata watu wanaobadilisha mifumo hiyo hawana hata shahada ya awali.
Kwa upande wa mwakilishi wa wanafunzi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa chuo hicho, Marrygorate Gervas, aliomba muda wa ufundishwaji wa masomo ya lugha uongezwe ili kuendelea kuzalisha wataalamu wa lugha kama Kifaransa, Kijerumani.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment