Tone

Tone
Home » » MIAKA 30 KISIWA HAKINA SHULE,WATOTO 300 HAWANA PAKUSOMA

MIAKA 30 KISIWA HAKINA SHULE,WATOTO 300 HAWANA PAKUSOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Ni wa familia za wavuvi
  DC, Mbunge wawaruka
Mmoja wa kina mama wenye watoto kisiwani Kome Mchangani akiwa katika mizunguko yake ya kila siku kisiwani humo hivi karibuni.
Wakati taifa likiendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), hali ni tofauti kwa watoto zaidi ya 300 wanaoishi katika Kisiwa cha Kome Mchangani kilichopo kwenye Ziwa Victoria, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza baada ya kutojengwa shule kwa zaidi ya miaka 30.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kwa zaidi ya wiki mbili kwenye kisiwa hicho umebaini kuwa tatizo hilo halitokani na kuwapo kwa hamasa ndogo ya elimu kwa wazazi wa watoto hao; bali ni matokeo ya utekelezwaji wa Sheria ya Uhifadhi Misitu ya Mwaka 2002, katika kifungu cha 26 kinachokataza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa majengo ya kudumu.

Kisiwa cha Kome Mchangani ni miongoni mwa visiwa vya Ziwa Victoria vilivyotangazwa na serikali kuwa hifadhi ya misitu.

Kiongozi wa wakazi na wafanyabiashara wa mazao ya samaki katika kisiwa hicho, Tibenda Luhuya, aliiambia NIPASHE kuwa wamejitahidi kupigania uwapo wa shule na huduma nyingine za jamii kisiwani humo kwa muda mrefu lakini hakuna wanachoambulia zaidi ya kuambiwa kuwa sheria za nchi haziruhusu.

"Tunaelezwa kuwa eneo lote la kisiwa (cha Kome) halitakiwi kuwa na majengo ya kudumu na hivyo, serikali haiwezi kutujengea shule wala zahanati kwa sababu kufanya hivyo ni kuvunja hizo sheria," alisema Luhuya.

Hata hivyo, wakati shule na majengo mengine ya kudumu yakizuiwa, serikali imeruhusu kuwapo kwa jengo la kudumu la vyumba vitatu ambalo linatumiwa na Kikosi cha Usimamizi wa Fukwe (BMU).

"Bado tunaendelea kuisihi serikali kuwa itujengee shule kwa ajili ya watoto wetu ambao wanaishia kuvua samaki tu na kukosa elimu ambayo ni haki yao ya msingi," aliongeza.

Anasema kisiwa hicho kina wakazi zaidi ya 5,000 na kinahesabika kipo katika Kijiji cha Buhama, Kata ya Nyakasasa, Tarafa ya Buchosa. Umbali wa kutoka kisiwa hicho mpaka Kijiji cha Buhama ambako kuna Shule ya Msingi ni zaidi ya kilomita tano.

Akieleza zaidi, Luhuya anasema kwa zaidi ya miaka 30 tangu wavuvi na wafanyabiashara wa mazao yatokanayo na samaki walipoanza kuishi hapo hawajawahi kuwa na shule na hivyo, baadhi ya wazazi hulazimika kuwapeleka watoto wao kwa ndugu, jamaa na marafiki wanaoishi nje ya kisiwa hicho ili wakasome.

Hata hivyo, anasema zoezi hilo limekuwa gumu kwa kuwa baadhi ya wazazi wakishawapeleka huko (kwa ndugu zao), huwa wanawatelekeza na matokeo yake watoto hao wanarudi wenyewe kwa kuomba nauli na wengine kuingia ndani ya boti inazokwenda kisiwani humo bila ya kuwa na nauli.

WATOTO, WAZAZI WANENA
"Inaniuma sana kujikuta naishi bila kujua kusoma na kuandika. Wazazi wangu ni wavuvi na wote hawakusoma. Lakini na mimi nitaishia kuwa mvuvi nisiyejua kusoma na kuandika kama wao kwa sababu hapa kwetu (Kome) hakuna shule," ndivyo anavyoanza kueleza mtoto mmojawapo kisiwani Kome Mchangani, John (11).

Ibrahimu anasema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisikia kwamba kuna harakati zinafanywa za kuiomba serikali iwajengee shule. Lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na anaamini kuwa yeye na watoto wenzake wote kisiwani humo hawatapata fursa ya kujua kusoma na kuandika.

"Mimi inaniuma sana kwa kutojua kusoma... huwa ninawaona baadhi ya watu wanasoma magazeti na vitabu, hasa wanaotoka Mwanza kuja kununua samaki huku kwetu. Lakini mimi sijui kusoma wala kuandika.Ninachokijua zaidi ni kuvua na kufanya kazi ya kusomba dagaa kutoka ziwani kuwaleta nchi kavu," anasema Ibrahim.

Mtoto aitwaye Yona, mwenye umri wa miaka 10, anasema kutokana na kisiwa hicho kukosa shule, wazazi wake walimpeleka Mwanza mjini kwa rafiki yao ili akasome huko, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu huko alikopelekwa, wenyeji hawakuipa shule nafasi na hata watoto wao (wa wenyeji) hawakuwa wakienda shule.

''Sasa nimerudi kwa wazazi wangu hapa kisiwani. Nimekaa wala sijui kama nitasoma... naendelea na kazi ya kibarua cha kusomba samaki kutoka katika mitumbwi ya wavuvi nyakati za jioni,'' alisema.

Tatu Kipile ni mmoja wa wakazi wa kisiwa cha Kome Mchangani. Anasema kuwa yeye ameshindwa kumpeleka shule mtoto wake anayeishi naye huko kutokana na kukosa fedha za kumsafirisha kutoka kisiwani humo na kumhudumia wakati anapokwenda kwenye eneo lenye shule.

"Nilihamia hapa (Kome) wakati mwanangu akiwa na miaka mitatu. Sasa ni zaidi ya mwaka wa tano niko hapa. Ninapenda sana mwanangu asome, lakini sina namna ya kufanya kwa sababu kisiwa hiki hakina shule na sina fedha za kumpeleka kwenye maeneo ya mbali yaliyo na shule za msingi," alisema mama huyo.

Hellen Cosmas alisema analazimika kumpangia chumba jijini Mwanza mtoto wake mwenye umri wa miaka 10 ili apate fursa ya kusoma, ingawa anasema bado kuna changamoto nyingi ya kutekeleza azima yake hiyo kwa sababu hana mwangalizi maalum.

"Hivi sasa nimemrudisha hapa kisiwani (Kome) kwa sababu mazingira ya kuishi Mwanza ni magumu. Hana mwangalizi na hivyo sasa niko naye hapa... haendi tena shule," alisema Hellen.

Sara Machera bado hajabahatika kupata mtoto. Hata hivyo, alisema kuwa hali iliyopo sasa ni ngumu kwa wazazi wa kisiwa hicho kutekeleza jukumu la kusomesha watoto wao kwavile hakuna shule. Aliongeza kuwa watoto wanaopelekwa kwa ndugu zao ili wasome ni kama huwa wanatelekezwa kwani uangalizi huwa mdogo.

Neema Abel ambaye pia bado hajapata mtoto anasema watoto kisiwani humo hukosa elimu kwavile hakuna shule na hivyo anaiomba serikali ifikirie kuwajengea shule ili kuokoa mamia ya watoto walio katika hatari ya kuwa wajinga, wasiojua kusoma wala kuandika.

VISIWA VINGINE
Tatizo la shule linalowakabilia wakazi wa kisiwa cha Kome Mchangani lipo pia katika visiwa vingine kadhaa vilivyomo kwenye Ziwa Victoria.
Mwanamama Agnes Joseph, mkazi wa kisiwa cha Ikulu alisema kuwa yeye ana watoto watano, na wote amewapeleka kwa mama yake ambako ni katika eneo lisilokuwa la kisiwa wilayani Sengerema ili wasome.

"Huwa ninawatembelea kila baada ya miezi miwili na kuwaachia fedha za matumizi... sitaki wanangu wakose fursa ya elimu," anasema Agnes.
Kiongiozi wa Kisiwa cha Ikulu Baharini, Juma, alisema watoto kukosa elimu na kuishia kuwa wavuvi kwa sababu ya kukosekana kwa shule ni janga kubwa kwao na taifa.

Alisema kwavile serikali inafahamu kwamba kwenye visiwa kuna mamia ya watu ambao ni Watanzania halisi, inapaswa kuchukua hatua sahihi ya kuwajengea shule.

Kiongozi wa Kisiwa cha Ito, Neema Elias, alisema eneo hilo lina wakazi (wavuvi) zaidi ya 500, lakini hakuna shule kwa ajili ya watoto wao.
Aliongeza kuwa tatizo la watoto kukosa elimu kwa sababu ya serikali kutokubali kujenga shule lipo pia katika visiwa vingine vingi miongoni mwa visiwa 35 vilivyopo katika Ziwa Victoria, hasa kwenye eneo la Wilaya ya Sengerema.

Alisema licha ya kukosekana shule katika eneo hilo, lakini pia wamepata maagizo ya serikali kwamba kamwe hawaruhusiwa kuishi kisiwani humo wakiwa na watoto wao.

"Hii siyo sawa.  Wazazi wanapozaa watoto wanalazimishwa kuwaondoa watoto kwa madai kwamba hakuna shule na tunatakiwa kuwapeleka kwa ndugu, jamaa na marafiki walio katika maeneo yenye shule, nje kabisa ya visiwa. Lakini hili limeshindikana... bado tunaishi na watoto wetu na matokeo yake wanakosa elimu," anasema.

OFISA ELIMU, MBUNGE
Akizungumzia tatizo la kukosekana kwa shule, Ofisa mtendaji wa Kata ya Nyakasasa, Mathayo Kanisiro alisema, eneo la visiwa hivyo ni msitu wa hifadhi na kwamba serikali imeagiza pasijengwe nyumba wala jengo lolote la kudumu.

Kanisiro alikiri kwamba hakuna namna ya kufanya, lakini amekuwa akistushwa na ukubwa wa tatizo kwani watoto wanaoishi na wazazi wao katika visiwa hivyo bila kupata haki yao ya msingi ya elimu imezidi kuongezeka.

Diwani wa Kata ya Nyakasasa, Avoid Geogratias, anasema eneo hilo la visiwa wanalokalia wavuvi na familia zao, lilitengwa kwa ajili ya hifadhi ya mistu miaka mingi iliyopita na kwamba, awali, wavuvi waliruhusiwa kuishi huko ili kulinda misitu huo dhidi ya watu waliokuwa wanapasua mbao.

Naye, kama ilivyo kwa Kanisiro, alisema hana namna yoyote ya kuwasaidia watoto hao ili wapate nafasi ya kusoma na kwamba, anajua kwamba watoto wamezidi kuwa wengi kama wanavyoongezeka wazazi wao (wavuvi).

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Sengerema, Juma Mwajombe, alisema kuwa siku za nyuma kulikuwa na utaratibu wa wa wazazi kuchangishana fedha kisha kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya visiwa. Lakini mpango huo ulifikia mwisho mwaka 2010 baada ya kutokea ajali ya kuzama kwa mtumbwi na wanafunzi 18 walipoteza maisha.

"Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, zoezi hilo lilisimamishwa na hadi sasa watoto wengi wameendelea kuishi visiwani bila kupata elimu," alisema Mwajombe, aliyeelezea wasiwasi mwingine kuwa huenda misitu itakuwa hatarini kwa sababu baadhi ya wakazi wa visiwani wataona hakuna haja ya kulinda misitu wakati watoto wao wakikosa elimu kwa kutojengewa shule kwa sababu ya zuio litokanalo na sheria ya kulinda misitu.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Sengerema, Consolata Magaka, alisema serikali inafahamu shida wanayopata wazazi na watoto walio kweney visiwa kama Kome Mchangani, lakini hakuna namna ya kufanya.

Alisema serikali haiwezi kupeleka huduma za shule kwa kuwa wananchi hao wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi wako aktika eneo la hifadhi ya misitu.
Mbunge wa jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema, Charles Tizeba, aliiambia NIPASHE kuwa, kama kuna mwananchi anayetaka kuendelea kukaa kisiwani (kama Kome) ambako ni hifadhi ya misitu, lazima amuondoe mtoto wake huko na kumrudidisha alikozaliwa ili ampatie fursa ya kusoma.

Alisema hawezi kuwatetea wananchi wake hao kujengewa shule visiwani, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya misitu ambayo inakataza kuwapo kwa majengo ya kudumu.

Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Focus Majimbi, alisema ni vigumu kujenga shule kwenye kisiwa cha Kome na visiwa vingine vya hifadhi ya misitu kwani sheria inazuia maeneo hayo (ya hifadhi ya misitu) kujengwa majengo ya kudumu. Aliitaja sheria hiyo kuwa ni namba 14, ya mwaka 2002, kifungu cha 26.

Majimbi alikiri kwamba suala la ukosefu wa elimu kwa watoto ni baya na lina athari kubwa. Alisisitiza kuwa, kwa kuzingatia sheria hiyo ya hifadhi ya misitu, maeneo ya visiwa hivyo hayatakiwi kujengwa shule wala jengo lolote la kudumu na kwamba serikali imeagiza kuhamisha watoto wote walioko huko ili wakasome katika maeneo mengine.

Hata hivyo, amri hiyo ya serikali ya kutaka watoto wanaozaliwa huko waondoshwe inakiuka sheria nyingine ya nchi; namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inalinda haki za watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Wilaya ya Sengerema ina ukubwa wa kilomita za mraba, 8,817 na kati ya hizo, kilomita za mraba 3,335 ni nchi kavu sawa na asilimia 38 na kilomita 5, 832 ni nchi kavu, sawa na asilimia 62.

Kwa mujibu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2010, wilaya hiyo ina watu 662,166 na kati ya hao, wanaume ni 335,756 na wanawake ni 326,410.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa