WANANCHI wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, wamepinga utaratibu wa
serikali kupitisha fedha za miradi ya maendeleo kwenye Kamati za
Maendeleo ya Kata (WDS), na kusema fedha hizo zinapaswa zipelekwe moja
kwa moja katika serikali za vijiji husika.
Walisema mfumo huo ni mbovu, na unachangia kuwepo kwa ufisadi na
kushindwa kutekelezwa kwa miradi kama ilivyopangwa katika bajeti ya
serikali, hivyo ni vema fedha hizo zikawa zinapelekwa kwenye akaunti za
vijiji vilivyopangiwa miradi.
Hayo yameelezwa juzi na washiriki wa mdahalo ulioandaliwa na Shirika
la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la TABCO, kupitia mradi wake wa
ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga bajeti ya serikali ngazi ya
vijiji na mitaa, iliyofanyika ukumbi wa Consolata mjini Nyanguge, Magu.
Wakichangia kwenye mdahalo huo uliowashirikisha wananchi kutoka kata
tatu za Kitongosima, Nyanguge na Mwamanga wilayani Magu,
waliwalalamikia wajumbe wa WDS kwa madai wengi wao hawawaelezi wananchi
fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya maendeleo ndani ya vijiji
vyao.
“Miradi mingi wananchi wanaona inajengwa tu. Utaona barabara
inatengenezwa au kisima, zahanati bila wananchi kushirikishwa wala
kuambiwa hizi hela zimetoka wapi. Hii yote inatokana na kamati za
maendeleo ya kata kuwa wasiri sana. Hawasemi wala kusoma mapato na
matumizi hawafanyi hivyo,” alisema.
Akizungumza katika mdahalo huo, Mkurugenzi wa TABCO, Keneth Edward,
alisema mamlaka zote lazima ziwashirikishe wananchi katika mipango yote
ya maendeleo, ikiwemo bajeti za vitongoji, mitaa na serikali za
vijiji.
“Sisi TABCO tunahitaji kuona kila mwananchi anashirikishwa katika
masuala yote ya kimaendeleo. Wananchi ndio nguzo ya maendeleo,
haiwezekani wawekwe kando kwenye mambo muhimu kama haya,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment