Tone

Tone
Home » » Sumaye ataka viwanda vya ndani vilindwe

Sumaye ataka viwanda vya ndani vilindwe

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema kuwa ni vigumu kuuondoa umaskini nchini kama serikali haitaongeza uuzaji wa bidhaa zake nje ya nchi.
Alisema serikali pia lazima ivilinde viwanda vyake vichanga dhidi ya ushindani wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje.
Wito huo aliutoa jana mkoani Mwanza, wakati akitoa mada ya ‘Ujenzi na Ukuzaji wa Uchumi Imara’ katika mkutano wa  Wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Alisema ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi utategemea sana na jinsi nchi husika itakavyouza nje bidhaa kutoka viwanda vyake hivyo ni vema serikali ikatoa ulinzi katika sekta binafsi.
“Nchi inatakiwa iuze zaidi nje kuliko inavyoagiza kutoka nje kwa nchi zetu maskini, hali hii ni kinyume kabisa, ndiyo maana umaskini hauishi,” alisema.
Alisema baadhi ya nchi za nje zimekuwa zikitoa upendeleo wa kisirisiri kwa bidhaa zao wanazopeleka nje ya nchi, jambo linalofanya uwepo ushindani usio halali kwa soko la ndani.
Aliongeza kuwa kigezo kimojawapo muhimu kinachotofautisha nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni uwepo wa viwanda vinavyozalisha bidhaa za kuuzwa katika soko la dunia.
Sumaye alisema kwa ukuaji endelevu wa uchumi lazima Tanzania ijenge na  kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani ili ziwe na ubora na wingi unaotosheleza ushindani katika masoko  ya nje.
“Tunahitaji utaalamu wa teknolojia za kisasa katika uzalishaji, rasilimali watu wenye utaalamu na ujuzi wa kutosha, zana za kisasa za uzalishaji na ujuzi wa masoko,” alisema.
Sumaye alisema nchi za Afrika zinapaswa kutunga  sera rafiki kwa maendeleo ya sekta binafsi na kulinda sekta changa isiuawe na ushindani usio halali kutoka nje.
“Ni lazima kuwe na sera ya makusudi ya kuongeza uuzaji nje wa bidhaa na huduma kama tunataka kujenga utajiri ndani ya nchi.
“Uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi  hujenga utajiri kwa kuuza bidhaa na huduma zake katika masoko ya nje. Hii ndiyo maana uwiano wa biashara ni muhimu sana,” alisema.
Alibainisha kuwa sekta binafsi kama kiongozi wa maendeleo ya uchumi endelevu ichukue nafasi yake na serikali ishirikiane nayo badala ya kuiona ni mshindani au adui kwake.
Sumaye alisema usindikaji wa kubadilisha bidhaa za mazao kuwa bidhaa za viwandani ndio mfumo unaotumiwa na mataifa yaliyoendelea wakati nchi nyingi zinazoendelea duniani hutegemea kilimo ambacho hushindwa kuyaongezea thamani mazao yanayozalishwa.
Alibainisha kuwa mazao yasiyoongezwa thamani yoyote hununuliwa kwa bei za chini na isiyotabirika, hivyo kuzifanya nchi maskini kupoteza sehemu kubwa ya biashara zao katika soko la kimataifa.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

1 comments:

Anonymous said...

Amakweli kila shabiki ni mjuzi kuliko kila mchezaji.Huyu mweshimiwa alipokuwa kwenye nafasi yake alikuwa hayaongelei haya, leo hii kawa mkosoaji na mshauri mkubwa!duu

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa