Home » » MBUNGE CCM AISHAMBULIA TUME YA KATIBA

MBUNGE CCM AISHAMBULIA TUME YA KATIBA

MBUNGE wa Kwimba (CCM), Shanif Mansoor, ameishambulia Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba. Akizungumza jimboni kwake juzi alipokutana na wazee na waganga wa tiba za asili katika Kata ya Mankulwe, alimtaka Warioba na wenzake kuacha mara moja kuwa wapiga debe katika vyombo vya habari kuhusu Serikali tatu.
Alisema wabunge wa CCM na baadhi ya viongozi, wanapinga kufanya kazi na rais asiye na jeshi ikiwa kutakuwa na Serikali tatu.

Aidha, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kutumia busara katika masuala mawili ya kuondoa kipengele cha Serikali tatu, kama hoja mpya au kusitisha uundwaji wa Bunge Maalumu la Katiba na kuanzisha kwanza mchakato wa kutafuta maoni ya Katiba ya Tanganyika.

“Mzee Warioba ana heshima zake na msomi mzuri, binafsi namheshimu lakini katika suala la Serikali tatu aliloliweka katika rasimu ya pili, inadhihirisha amefeli.

“Uzee wake unaonekana kumpeleka pabaya, kwa sababu baada ya kukabidhi rasimu ya pili kwa Rais Kikwete, ameendelea kuwa mpiga debe na mshawishi mkubwa kupitia vyombo vya habari.

“Kazi aliyopewa Jaji Warioba amekwishaimaliza kwa kuiharibu, sasa anapaswa kuwaachia wabunge na wananchi kutekeleza kile kinachofuata,” alisema Mansoor.

Aliwataka wananchi kukataa mfumo wa Serikali tatu, kwa kuwa hauna tija kwa nyakati hizi na kuongeza wabunge wa CCM wamejipanga kupinga kwa nguvu zao zote ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Alisema inaonekana wazi kuna kitu ndani ya Katiba hiyo ambacho Jaji Warioba anakitaka kutokana na ushawishi anaouendeleza sasa na kama hakuna, basi hakufikiri kwa mapana zaidi kuweka Serikali tatu.

Alisema hatua iliyopo sasa ya kutafuta Katiba Mpya ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, ni sawa na kufunga ndoa wakati bibi harusi hayupo.

Alisema Katiba ya Watanganyika haiwezi kupatikana kutokana na maoni na yaliyochangiwa na Wazanzibari.

Alisema inawezekana wakati wa kutafuta Katiba ya Tanganyika, wananchi wa Tanganyika wakakataa Muungano kitendo kinachoweza kuifuta Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayopatikana kwa gharama kubwa.

“Ni ushauri kwa Rais Kikwete, ni vema akasitisha mchakato huu tuanze upya kutafuta maoni ya Katiba ya Tanganyika kwanza, ndipo hii ya Muungano ifuatie kwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, hawawezi kushiriki Katiba ya Tanganyika.

“Namshangaa Jaji Warioba kusema Katiba ya Tanganyika inaweza kutengenezwa kwa miezi mitatu, kwa sababu kazi kubwa ameifanya, binafsi nasema haiwezekani kuwa na Katiba ya Tanganyika yenye maoni ya Wazanzibari, wakati Wabara hawachangii ya Zanzibar,” Mansoor.

Alisema Bunge Maalumu la Katiba linaweza kuwa sehemu ya matumizi mabaya ya fedha, kwa kuwa kinachofanyika hakina manufaa kama mfumo wa Serikali tatu utakuwapo.

Alisema kitakuwa ni kituko cha dunia Tanganyika yenye watu zaidi ya milioni 45, kuwa na rais asiye na jeshi huku visiwa nyenye watu milioni tatu vikiwa na jeshi.

Alisema idadi ya maoni ya watu waliohojiwa na kusema kuwapo na Serikali tatu ni ndogo, ambayo haiwezi kutengeneza Katiba ya Tanganyika na kuwataka wananchi kuunga mkono msimamo wa CCM.

Alisema anashangazwa na kitendo cha Jaji Warioba kujigeuza kuwa mchumi na mtabiri, kwa kusema hakuna gharama katika kuendesha Serikali tatu ukizingatia Tanzania bado ni masikini.

Chanzo:Mtanzania 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa