Tone

Tone
Home » » Idadi waliokamatwa mauaji kigogo CCM yaongezeka

Idadi waliokamatwa mauaji kigogo CCM yaongezeka

Clement Mabina
 
Idadi ya watu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, Clement Mabina imeongezeka kutoka saba hadi 10. 
Habari kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa zimeeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Kisesa kwa ajili ya kuhojiwa.

 “Zaidi ya watuhumiwa 10 tunawashikilia hadi sasa  kwa ajili ya mahojiano. Hadi jana (juzi) mchana   tulikuwa nao watuhumiwa saba,” alisema afisa mmoja wa jeshi hilo kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Kamanda  wa Polisi mkoani  hapa, Valentino  Mlowola, hakupatikana ofisini kwake wala kwa  njia ya simu yake ya mkononi kuzungumzia suala hilo.

Mara zote simu yake iliita bila kupokelewa na hata  alipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) hajajibu.

 Katika hatua nyingine,  Katibu wa CCM Wilaya ya Magu, Isack Zablon, alisema bado ofisi haijapata  taarifa rasmi kuhusu majina ya viongozi wa kitaifa  wa chama na serikali watakaohudhuria mazishi ya Mabina yaliyopangwa kufanyika kesho.

“Bado sijapata taarifa kuwa ni viongozi gani wa kitaifa watakaohudhuria kwenye mazishi. Sasa hivi  tupo kwenye misa,” alisema Zablon.

Mabina, ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa, wilayani Magu, aliuawa Jumapili wiki iliyopita, majira ya asubuhi baada ya kushambuliwa na wanakijiji akidaiwa kumuua kwa risasi mtoto  mwenye umri wa miaka 12 kutokana  na mgogoro  wa ardhi baina yake na wakazi wa kijiji hicho.

 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa