Tone

Tone
Home » » Uhaba wa mwalimu nchini kuisha 2015

Uhaba wa mwalimu nchini kuisha 2015

TATIZO la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi nchini litamalizika mwaka 2015, imeelezwa. Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema tatizo hilo litamalizika Serikali itakapokamilisha mpango wa kuziunganisha taasisi za elimu za vyuo vikuu na sekondari zote nchini na mkongo wa taifa.

Alisema hatua hiyo itasaidia elimu nchini itolewe kwa usawa. Profesa Mbarawa aliyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Mwanza kujionea shughuli ya ujenzi wa mkongo wa taifa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.

Katika ziara hiyo, waziri pia aliwahamasisha wafanyakazi wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) mkoani Mwanza kufanya kazi ya kuwashawishi wateja kujiunga na huduma za mkongo.

Alisema lengo kubwa la mkongo wa taifa ni kuhakikisha pia linapunguza tatizo kubwa la walimu wa masomo ya sayansi ifikapo mwaka 2015 baada ya taasisi za elimu kuunganishwa. Waziri alisema elimu ya masomo ya sayansi nchini kote itakuwa ikitolewa kwa njia ya mawasiliano jambo ambalo litasaidia kumalizika haraka uhaba wa walimu nchini.

“Mpango huu tunatarajiwa utakuwa umekamilika nchini kote muda mufupi ujao na tayari maeneo yote yamepitiwa na mkongo huu na TTCL kwa kushirikiana na Wizara yangu tunaendelea na kuwaunganisha wateja ili kupatikana huduma ambayo italeta mafanikio,” alisema.

Alisema kwa sasa Serikali ina mpango wa kwenda katika shule zote na hadi sasa shule 40 zimekwiisha kupatiwa mawasiliano hayo.

“Mwakani zitakuwa 150 na zitakapokamilika mwalimu mmoja ataweza kufundisha wanafunzi nchi nzima kwa kipindi kimoja na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa walimu,” alisema.
Chanzo: Rai

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa