Tone

Tone
Home » » Serikali kutumia wataalamu tatizo la mipaka Mwanza

Serikali kutumia wataalamu tatizo la mipaka Mwanza

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeamua kutuma wataalamu kwa ajili ya kushughulikia utata wa mipaka baina ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Akizungumza na Rai, Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula, alisema baada ya TAMISEMI kukutana na uongozi wa Jiji la Mwanza, aliokuwa ameuongoza pamoja na uongozi wa Manispaa ya Ilemela uliokuwa ukiongozwa na Meya Henry Matata, ilikubaliwa na pande zote kuwa wizara itume wataalamu kwa ajili ya kuja kushughulikia tatizo hilo.

Alisema safari yao TAMISEMI, imekuwa na manufaa makubwa na kueleza kuwa utata huo utafikia mwisho baada ya wataalamu kufika jijini Mwanza na kutembelea jiji la Mwanza pamoja na Manispaa ya Ilemela na kutoa mapendekezo kwa ngazi za juu.

“Tumekutana na viongozi wa TAMISEMI pamoja na wadau wengine, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ambaye amehamishiwa jijini Dar es Salaam, tunamalizia mambo fulani na muda si mrefu wataalamu watafika jijini Mwanza kwa ajili ya kutatua utata huo wa mipaka,” alisema Meya Mabula.

Hivi karibuni akiwa katika ziara ya siku saba mkoani Mwanza, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa Halmashauri ya Jiji ili iweze kukamilika na kuwa na sifa ya kuitwa jiji, lazima mipaka ya Manispaa ya Ilemela ijumuishwe.

Alisema wakati akiridhia kuanzishwa kwa Manispaa ya Ilemela na muundo wake, alitoa maelekezo juu ya mipaka ya Manispaa hiyo kuwa sehemu ya jiji la Mwanza na si vinginevyo na kueleza kuwa bila Ilemela Jiji la Mwanza halina sifa hiyo.
Chanzo: Rai

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa