Tone

Tone
Home » » RAIS DR. JAKAYA KIKWETE AZINDUA MRADI WA KUFUA UMEME, MAELFU YA WAKAZI WA MWAZA WAJITOKEZA KUMSIKILIZA!

RAIS DR. JAKAYA KIKWETE AZINDUA MRADI WA KUFUA UMEME, MAELFU YA WAKAZI WA MWAZA WAJITOKEZA KUMSIKILIZA!


 Maelfu ya wakazi wa Mwanza na miji ya jirani wakimsikiliza Rais Kikwete katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo jioni.

 Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia maelfu ya wakazi wa Mwanza na miji ya jirani katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo jioni.Rais Kikwete yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo Picha na Freddy Maro
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunua kitambaa na kubonyeza kitufe kuashiria kuzindua mradi wa kufua umeme wa megawati 60 huko Nyakato,Mwanza leo asubuhi.Kushoto ni Waziri wa Nishati na madini Profesa Sospeter Muhongo.Uzinduzi wa mitambo hiyo ni sehemu ya ufumbuzi wa tatizo la umeme uliokuwa unaikabili kanda ya ziwa.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mitambo ya kufua umeme wa megawati 60 muda mfupi baada ya kuzindua mitambo hiyo huko Nyakato Mwanza leo. 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete (kulia akiwa na mavazi maalumu) akikagua jengo la upasuaji katika hospitali ya wilaya ya Nyamagana,Mkoani mwanza leo mchana.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Septemba 8, 2013, amezindua mtambo wa kufua umeme kiasi cha megawati 60 katika eneo la Nyakato mjini Mwanza, umeme ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza shida ya umeme katika Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Aidha, Rais Kikwete ameiangiza Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza mara moja maandalizi ya kupeleka umeme kwenye machimbo ya madini ya nikeli yaliyoko Kabanga, Ngara, Mkoa wa Kagera.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaharakisha mipango ya kujenga reli hadi kwenye eneo hilo kama maandalizi ya kuanza kuchimbwa kwa madini hayo ambayo ni mazito na kuyasafirisha kwa barabara kwenda bandarini Dar Es Salaam kutaharibu kwa haraka barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua mtambo huo, Rais Kikwete  ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuharakisha mipango ya kuunganisha eneo la Kabanga, Ngara, Mkoani Kagera kwenye Gridi ya Taifa ili uzalishaji wa madini ya nikeli usije kukwamishwa na ukosefu wa umeme. Amesema kuwa mgodi huo utahitaji umeme mwingi kiasi cha megawati 40.
Rais amesema kuwa Serikali yake itahakikisha inafikisha reli kwenye eneo la Kabanga mapema ili kuhakikisha kuwa nikeli inayozalishwa inasafirishwa kwa reli badala ya barabara. Amesema kuwa madini hayo ni mazito mno na kuyasafirishwa kwa barabara kutaharibu kabisa na katika muda mfupi barabara ambazo zinajengwa nchini kwa gharama kubwa.
Mtambo wa Umeme wa Nyakato wenye uwezo wa kuzalisha megawati 60 ulianza kujengwa mwaka jana, 2012, baada ya Serikali ya Tanzania kutiliana mkataba wa ujenzi na Kampuni ya Semco and Rolls Royce ya Norway mwaka 2011 wakati maandalizi ya ujenzi huo yalipoanza.
Gharama za ujenzi wa mtambo huo ambazo ni sh bilioni 130 (Euro milioni 48.7 na dola za Marekani 15.9) zimelipwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi kwenye sherehe ya uzinduzi huo, Rais Kikwete amesema kuwa umeme siyo anasa bali ni moja ya vigezo vya msingi na muhimu kabisa vya maendeleo.
“Vipo vigezo vingi vya maendeleo ya nchi na binadamu, lakini moja ya vigezo hiyo ni umeme. Na ukiangalia matumizi ya umeme kwa kila nchi yanaonyesha kiwango cha maendeleo cha nchi hiyo. Katika Marekani, kwa mfano, kila mwananchi anatumia kiasi cha kilowati 12,000 kwa wastani. Sisi katika Tanzania ni kilowati 89 tu na wastani wa Bara la Afrika ni kilowati 150,”  amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nc hi yetu ya Tanzania ina umeme kiasi cha megwati 1,450 tu wakati katika Afrika Kusini ni megawati 45,000 na unaweza kuona tofauti ya maendeleo. Hivyo, ni muhimu sana kwetu kuongeza kiwango cha kuzalisha umeme katika nchi yetu.”
Katika siku ya tatu ya ziara yake kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza, Rais Kiwete pia amefungua Kituo cha Polisi cha Nyakato ambacho kimegharimu sh milioni 450, Serikali ikiwa imechangia kiasi cha asilimia 20 cha gharama hizo.
Kituo hicho cha kisasa kilianza kujengwa mwaka 2003 lakini ujenzi wake ukawa unakwamakwama kutokana na ukosefu wa bajeti hadi uongozi wa polisi wa Mkoa wa Mwanza ulipoamua  kukijenga kituo hicho kwa njia ya kuishirikisha jamii na ikaundwa Kamati ya Ujenzi chini ya uenyekiti wa Bwana Alfred Wambiura.

Akizungumza kwenye sherehe ya ufunguzi wa kituo hicho, Rais Kikwete ameahidi kuwa atajenga nyuma moja kwa ajili ya mkazi ya polisi. Kituo hicho kina jumla ya askari polisi 65.
PICHA NA IKULU

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa