Tone

Tone
Home » » Agizo la Pinda kuhusu mali za Nyanza lapuuzwa

Agizo la Pinda kuhusu mali za Nyanza lapuuzwa

AGIZO la Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuutaka uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ukae na uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (NCU) kuhusu kuuzwa kwa ghala la NCU linasemekana limepuuzwa.

Habari zinasema uongozi wa Nyanza umeamua kumuandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri kutaka kusimamisha mara moja hatua ya kumpatia hati ya umiliki wa kiwanja namba 104 mfanyabiashara wa jijini hapa, Amos Njile hadi pande zote tatu zitakapoketi kutatua tatizo hilo.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na uongozi wa NCU kwenda kwa Mkurugenzi wa jiji la Mwanza ambayo Mtanzania imeiona, NCU inadai baadhi ya maofisa wa ardhi wamekuwa wakiandaa hati kwa ajili ya kumlikisha mfanyabiashara huyo eneo hilo.

Barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa NCU imeeleza kuwa eneo lililopo ghala lililouzwa na mahakama kwa Sh milioni 62 lina thamani ya Sh bilioni 1.7.

Katika eneo hilo pia kuna ghala jingine dogo na mzani, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 300.

Awali baada ya Mahakama kutoa amri ya kuuzwa kwa ghala hilo lililopo eneo la viwanda Igogo, pande zote zilikubaliana kwa vile katika eneo hilo kuna maghala na mali nyingine za NCU, mfanyabiashara apimiwe mita 1.5 kila upande lakini alikataa na ikakubaliwa apimiwe mita 5 kila upande katika eneo hilo.

“Mnunuzi alitaka kupimiwa mita 25 lakini NCU tulikataa na ndipo tulipokwenda kumuona Waziri Mkuu ambaye aliagiza suala hilo lipatiwe ufumbuzi na kupatiwa taarifa, lakini hakuna kikao kilichoketi na badala yake tunaona viongozi wa jiji wakiendelea na taratibu za kumpatia hati Njile hivyo tunaomba hatua hiyo isimamishwe,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Mwenyekiti wa NCU Leonard Bugomola alisema hayuko tayari kuona mali za wana ushirika zinapotea bure. Aliwatuhumu baadhi ya watendaji wa Serikali kwa kuwa nyuma na uovu huo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa