Home » » WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA

Na John Maduhu, Mwanza
MKUU wa Maabara ya Samaki Kanda ya Ziwa, Stephen Lukanga, amewataka wafanyabiashara katika Soko la Kimataifa la Mwaloni, kuzingatia sheria zilizowekwa na kuacha kugomea sheria hizo.

Akizungumza na MTANZANIA juu ya kuwapo kwa mgomo katika soko hilo wa kusafirisha samaki na mazao yake kwenda nje ya nchi kupinga tozo ya Sh 50,000 inayotozwa kwa ajili ya kugharamia sampuli za samaki katika maabara hiyo, alisema waliamua kuweka tozo hiyo, kwa ajili ya kulinda soko pamoja na ubora wa bidhaa zinazotoka Tanzania kwenda nje ya nchi, ambapo sampuli za samaki wanaotaka kusafirishwa lazima kwanza zipimwe katika maabara hiyo iliyopo eneo la Nyegezi.

Alisema ameshangazwa na mgomo wa wafanyabiashara hao na kama wana malalamiko, wanapaswa kuandika barua rasmi kwake na wizara husika.

“Huwezi ukasafirisha samaki na mazao yake kwenda nje ya nchi, bila kujua ubora wake ni muhimu wafanyabiashara wakalielewa hili na kama sheria ina upungufu wanapaswa waje tukae pamoja na kujadiliana,” alisema Lukanga.

Alisema suala la uchukuaji wa sampuli za samaki kabla hazijasafirishwa baada ya kuthibitishwa ubora wake, halina mjadala na kuwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria za nchi.

“Tutaendelea kuchukua sampuli na kutoa vibali kwa wasafirishaji wa samaki na mazao yake, wafanyabiashara wanapogoma haiwasaidii, badala yake wanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa,” alisema Lukanga.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa