na Jovither Kaijage, Ukerewe
WAKUU na wasimamizi wa kaya katika wilaya ya Ukerewe, Mwanza wametakiwa kuandaa na kutunza kumbukumbu zilizo sahihi za watu waliolala katika kaya zao usiku wa kuamkia kesho ili kuondoa mkanganyiko wakati wa kutoa taarifa hizo kwa karani wa sensa.
Mwenyekiti wa kamati ya sensa ya watu na makazi ya wilaya hiyo, Mary Tesha alisema hayo jana katika Kijiji cha Bwisya kisiwani Ukara wilayani hapa, alipokuwa akihamasisha wananchi kushiriki katika sensa.
Alisema, wakati zoezi hilo linatarajia kuanza usiku wa kuamkia leo, ni vema wananchi wakatambua kuwa na kumbukumbu sahihi za watu waliolala katika kaya zao usiku huo.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa karani na kwa wahusika wengine wa zoezi hilo ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Kwa maelezo yake serikali imejipanga ili kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa makarani na wasimamizi wa zoezi hilo.
Alitaka wananchi watambue kuwa sensa ni muhimu kwa taifa lolote lenye nia ya kuhudumia vyema wananchi wake.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment